Thursday, May 22, 2014

MTOTO AFICHWA KWENYE BOKSI KWA MIAKA MINNE PASIPO KUFANYIWA USAFI WALA KUPEWA HUDUMA YOYOTE

 

Tukio hili limetokea mkoani Morogoro katika kata ya Kiwanja cha ndege ambapo mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Mariamu Saidi ametuhumiwa kutenda kosa la kumficha mtoto wa dada yake ambaye ameyefariki. Mtoto huyo amefichwa kwenye boksi hilo kwa miaka minne.

Siri hii ilifichuka baada ya majirani wa mariamu kwenda kutoa ripoti kwa afisa mtendaji wa kata hiyo ya Kiwanja cha ndege, Dia Zongo, kuhusu mtoto huyo Nasra Rashidi kuto kupewa haki za kibinadamu ikiwemo kufanyiwa usafi.

Dia Zongo alikwenda kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa mtaa na kuongozana hadi nyumbani kwa Mariamu ambapo wakati wanafanya naye mahojiano mtoto Nasra alipiga chafya kutokea ndani, ndipo walipoingia na kumkuta mtoto huyo akiwa kwenye boksi. Mtoto huyo alikuwa ametapakaa uchafu mwilini ukiwemo wa haja kubwa na ndogo alizokuwa anajisaidia. Bi.Mariamu alipohojiwa alisema mara ya mwisho kumuogesha mtoto huyo ilikuwa mwakajana mwezi Julai.

Wananchi walifika nyumbani hapo huku wakiwa wameshika mawe na fimbo na kuanza kumshushia kipigo mwanamke huyo kwa hasira. 

Muda mfupi baadae askari polisi walifika na kumpeleka kwenye ofisi ya kata, kisha baadaye wakampeleka kwenye kituo kikuu cha polisi cha mkoa wa Morogoro na kumsweka rumande.

Kamanda wa mkoa huo Bwana Leonard paulo, amesema kuwa wanaendelea kukusanya taarifa hizo pamoja na kumfanyia utafiti wa kitabibu mtoto Nasra kabla ya kuchukua hatua yoyote.
____________________________________________________________________________________________________________