Tuesday, May 20, 2014

MWANANCHI: Wagonjwa walalamika kulazimishwa kulazwa Amana

“Vipimo vinatolewa bure kwa wagonjwa wote wanaokuja kupima hospitalini hapa na tunawaomba wananchi, anayejisikia ana dalili za ugonjwa huu aje mara moja,” .PICHA|MAKTABA 

Kwa ufupi
Ni katika Hospitali ya Amana, wasema asiyelazwa anadaiwa Sh30,000. Mganga Mfawidhi atoa maelezo.

Dar es Salaam. Licha ya Serikali kutangaza kuwa matibabu ya homa ya dengue ni bure, inadaiwa kuwa baadhi ya watoa huduma katika Hospitali ya Amana wamekuwa wakiwatoza wagonjwa Sh30,000 huku wengine wakitakiwa kulazwa kabla ya kupimwa na baadhi wakiambiwa vifaa vimekwisha.

Hayo yanadaiwa kutokea wakati Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk Gilbert Ngua alinukuliwa Mei 16, mwaka huu akisema hakuna tatizo hilo kwani ilikwishapokea vipimo 100 vya ugonjwa huo vilivyokuwa vimetumika ni 44 na kusisitiza kwamba wagonjwa wanapimwa bure.

“Vipimo vinatolewa bure kwa wagonjwa wote wanaokuja kupima hospitalini hapa na tunawaomba wananchi, anayejisikia ana dalili za ugonjwa huu aje mara moja,” alisema Dk Ngua.

Hata hivyo, mmoja wa wagonjwa, Sarah Mwendapole alisema jana kuwa mmoja wa watoa huduma kitengo cha maabara aliwatangazia kuwa vifaa hivyo vimewaishia huku wengine wakielezwa kuwa utaratibu uliopo ni kwamba wanatakiwa walazwe ili vipimo vyao vichukuliwe wakiwa wodini.

“Nimeandikiwa niende maabara nikapime kipimo cha dengue lakini nilipofika nimeelezwa kuwa nitoe Sh30,000 lakini baada ya kuona hiyo hela sina ndipo wakaniambia vifaa vimeisha halafu kuna utaratibu anayeandikiwa kipimo hicho aende akalazwe vipimo vitatolewa akiwa wodini,” alisema Mwendapole.

Mgonjwa mwingine, Abdallah Sayuni alisema aliandikiwa kipimo hicho Jumamosi lakini alitakiwa akalazwe na kipimo kitachukuliwa akiwa wodini.

Akizungumzia madai hayo, mhudumu mmoja wa maabara ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema mgonjwa anayeandikiwa kipimo cha dengue lazima alazwe na vipimo vyao vitachukuliwa wakiwa wodini.

“Mgonjwa anayeandikiwa kipimo cha Dengue lazima akalazwe halafu vipimo vyao vitachukuliwa wakiwa wodini huo ndiyo utaratibu uliopo sasa,” alisema.

Hata hivyo, kauli hiyo ilipingwa na Dk Ngua ambaye alisema wahudumu wanaowataka wagonjwa waliokwenda kupima dengue walazwe kabla ya kuchukuliwa vipimo vyao, ni kosa na analifanyia kazi suala hilo.

“Mgonjwa anayelazwa kabla ya kupima ni yule mwenye dalili zote za ugonjwa huo na amezidiwa. Analazwa huku vipimo vyake vikichukuliwa akiwa wodini si kwa wagonjwa wote,” alisema Dk Ngua.

Alisema tangu Ijumaa hadi jana, wagonjwa wapya waliopokewa katika hospitali hiyo walikuwa 44, kati ya hao, 22 waligundulika kuwa na dengue, sita walilazwa na wengine waliruhusiwa kurudi nyumbani.