Saturday, July 11, 2015

Moto wauwa watoto wawili na kujeruhi wilaya ya Muheza.


Watoto wawili wa familia moja wamefariki dunia huku baba yao akijeruhiwa vibaya na kulazwa katika Hospitali teule ya wilaya ya Muheza kufuatia nyumba yao kuteketea kwa moto baada ya mafuta ya Petrol yaliyokuwa yamehifadhiwa katika nyumba hiyo kulipuka.

Wakizungumza katika eneo la tukio lililopo kijiji cha Songa mama mwenye nyumba iliyoteketea kwa moto pamoja na mashuhuda wa kijiji cha Songa Batini kilichopo kata ya Songa wilayani Muheza,wamesema moto huo umesababisha vifo vya watoto wawili wenye umri wa miaka 4 na 5 waliokuwa wakicheza ndani ya nyumba hiyo ambao wamefahamika kwa majina ya Mariam Zubeir,Neema Zubeir ambao wamefariki dunia na baba yao Zubeir Athuman ambaye amelazwa katika hospitali teule ya wilaya ya Muheza akiendelea na matibabu.
 
Akielezea jinsi walivyofanya jitihada za kuuzima moto huo ili kuokoa maisha ya watoto hao,mzee wa kijiji aliyeshiriki kuuzima moto huo Aweso Bakari amesema walilazimika kutumia maji ya msikitini ili kuokoa maisha ya watoto hao lakini bahati mbaya walifunikwa na bidhaa zilizokuwa zikiteketea kwa moto.