Akizungumza na waandishi wa habari visiwani Zanzibar jana kuhusu uwamuzi wa Profesa Lipumba kujiuzuru uenyekii wa chama hicho, Kaimu mkurugenzi wa mawasiliano na habari wa Cuf, Ismail Jussa Ladhu, alisema wameupokea na wanaheshimu mawazo yake ya kujiuzuru.
Alisema kiongozi huyo
ametumia uamuzi wake wa kidemokrasia na kwamba hatua hiyo aliyoamua hajakosea
na wala chama hakitatetereka kutokana na kujiuzulu huko.
Alisema Cuf inafahamu
mchango wake mkubwa kwa chama hicho kwani amekifanyia kazi kubwa kukiimarisha
na kukuza demokrasia ya nchi.
“Tunathamini kazi yake,
tutaendelea kumheshimu kwa utumishi wake mkubwa kwa chama chetu na nchi yetu na
tunamtakia kila la kheri katika mipango yake ya baadaye,” alisema Jussa.
Hata hivyo, Jussa alisema
kuondoka kwa kiongozi huyo kutaacha pengo hasa katika kipindi hiki cha kuelekea
uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu, lakini chama hicho
hakitayumba na kitaendelea kuwa ndani ya Ukawa ili kuhakikisha CCM inaondoka
madarakani.
Alisema kuwa katika
historia, Cuf imepita katika dhoruba na misukosuko mingi, lakini mara zote
imeonyesha uwezo mkubwa wa kuihimili na kukabiliana na athari zake.
VIKAO VYA DHARURA
VYAITISHWA
Alisema kufuatia hatua ya
Profesa Lipumba kujiuzulu, Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif, ameagiza
kuitishwa kwa vikao vya dharura vya Kamati ya Utendaji ya Taifa na Baraza Kuu
la Uongozi la Taifa Agosti 9, mwaka huu ili kujadili hatua hiyo na kufanya
maamuzi juu ya hatua muafaka zinazopaswa kuchukuliwa hadi hapo chama
kitakapomchagua mwanachama mwingine kujaza nafasi hiyo ya Mwenyekiti.