Tuesday, September 22, 2015

Hujuma Nzito Yaibuka Ndani ya Kambi ya Dr. Magufuli. HABARI KAMILI BOFYA HAPA=>

Hatimaye mgombea Urais kwa tiketi ya chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk, John Magufuli, ameibuka hadharani na kuzungumzia tatizo la kuwapo kwa baadhi ya wafuasi wa Chama chake kuhujumu kwa kuunga mkono harakati za upinzani.

Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli
Akizungumza kwenye viwanja vya Zimbiilo, Wilaya ya Muleba Kusini jana, Magufuli alisema anatambua kuwapo kwa baadhi ya wanaCCM wanaojionyesha kumuunga mkono nyakati za mchana lakini inapofika usiku hubadilika na kuwaunga mkono wapinzani.

“Naomba na nyinyi msiniangushe maana wengine mchana mnakuwa CCM, usiku mnahamia vyama vingine, mimi nina moyo kama nyie jamani msiponichagua nitakwazika sana Wanamuleba,” alisema Magufuli.

Hivi sasa, Magufuli amekuwa akichuana vikali na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anaeywakilisha pia muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya NLD, NCCR-Mageuzi na Chama cha Wananchi (CUF). Wote wawili wamekuwa wakivutia maelfu ya wananchi karibu katika kila mikutano yao ya kampeni kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 25.

Kadhalika, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Abdalah Bulembo, alizungumzia pia tatizo hilo la kuwapo kwa wanachama wa CCM  ambao wamekuwa wakisaidia wka kificho kampeni za mgombea urais kwa tiketi ya Ukawa, Lowassa.

Bulembo alifichua hayo wakati akizungumza kwenye mkutano wa kumnadi Dk. Magufuli katika Jimbo la Bukoba Vijijini.

Akieleza zaidi, Bulembo alisema ana ushahidi kwamba ziara ya Lowassa mkoani humo iliratibiwa na baadhi ya viongozi wa chama hicho na hivyo akawataka kuamua moja, ama kuitumikia CCM kwa dhati au kuondoka CCM mara moja na kumfuata Lowassa. “Msidhani hatuwafahamu. Mikakati yote na namna mnavyofadhili Ukawa na Lowassa tunafahamu, tena tunawafahamu kwa majina na nawaambia ole wenu... msipoondoka wenyewe, tutawafukuza baada ya Dk. Magufuli kushinda,” alisema Bulembo ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM.

“Anayempenda Lowassa na Ukawa avue magwanda ya CCM na awafuate huko. Hatutaki watu ambao mchana ni CCM usiku ni Lowassa… hili ni gari kubwa. Wengine wanashuka, wengine wanapanda,” alisema Bulembo.

Alisema yeyote mwenye kinyongo na CCM hafai kubaki ndani ya chama hicho kwa sababu (chama hicho) kina wanachama wengi na hakiangalii uwezo wa mtu kifedha.

“Tunawajua mnaomng’ang’ania Lowassa. Lakini nawahakikishia kuwa mtalia baada ya uchaguzi wa mwaka huu...  mnajifanya CCM lakini mnafadhili upinzani,  mwisho wenu unakuja,” alisema Bulembo.
Chanzo: Nipashe