Thursday, October 22, 2015

Mkuu wa Shule matatani kwa mapenzi na wanafunzi wake

MKUU wa Wilaya ya Mkalama mkoani Singida, Christopher Ngubiagai ameagiza Mkuu wa Shule ya Sekondari Chemichem wilayani humo, Juma Makoro kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kutokana na tuhuma za kufanya mapenzi na wanafunzi wake.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo kumwandikia barua ya kumsimamisha kazi mwalimu huyo kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili .
Vile vile ameagiza Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kufuatilia suala hilo. Ngubiagai alitoa agizo hilo juzi wakati wa kikao cha pamoja baina ya Watendaji wa Vijiji, Kata, Tarafa na Waratibu Elimu wa kata wa halmashauri hiyo na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya kilichofanyika mjini Nduguti.
Alisema kuwa vitendo viovu vya mkuu huyo wa shule viligundulika baada ya wanafunzi kulalamika kwa wazazi wao juu ya vitendo hivyo na wazazi kuamua kulifikisha suala hilo kwenye mamlaka za juu. “Haiingii akilini jinsi ambavyo mwalimu huyu alivyokuwa akiwadhalilisha wanafunzi wake wa kike kijinsia.
Tunaambiwa mwanafunzi akimpelekea madaftari kabla hajayapokea anamwambia mwanafunzi ambusu kwanza,” alisema Ngubiagai huku akionesha kuudhiwa na jambo hilo. “Mwalimu ni mzazi wa pili, ndivyo tunavyoamini.
Sasa huyu mzazi akifikia hatua hiyo huyo mwanafunzi atapata malezi ya aina gani? Ni jambo la aibu sana na ni kinyume na maadili ya taaluma ya ualimu. Kamwondoeni huyo wanafunzi wasome kwa amani,” aliagiza.