Wednesday, December 9, 2015

NEWS: Atakayechafua Mazingira Atakumbana na Faini ya 50,000/=

HALMASHAURI ya Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa imeonya kuwa itatoza faini ya Sh 50,000 kwa wakazi wa mjini Sumbawanga watakaobainika kutiririsha maji machafu ili kuhakikisha manispaa hiyo inabaki kuwa safi na salama.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Manispaa ya Sumbawanga, Hamidu Njovu alisema hiyo ni miongoni mwa mikakati iliyojiwekea katika kutekeleza agizo la Rais John Magufuli ambalo linawataka wananchi nchini kuadhimisha sherehe za Uhuru kwa kufanya usafi katika maeneo hayo wanayoishi au kazini.
Maadhimisho ya sherehe za Uhuru yanahitimishwa leo nchini kote kwa wananchi kufanya kazi tofauti na ilivyozoeleka tangu nchi hii ijipatie Uhuru wake miaka 54 iliyopita, ambapo shughuli hii imekuwa ikipambwa na gwaride kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
“Faini ya Sh 50,000 itatozwa kwa wale wote watakaobainika wakititirisha maji machafu katika makazi yao … kwani watakuwa wamekiuka Sheria ya Usafi na Mazingira za Halmashauri ya Mwaka 2008,” alisisitiza.
Pia amewaagiza walimu wakuu na wakuu wa shule za kutwa na wanafunzi wao katika manispaa hiyo kuhakikisha kuwa leo wanakuwa katika maeneo yao ya kazi (shuleni) na kuhakikisha wanashiriki katika zoezi la usafi kwa kuyaweka mazingira ya shule zao katika hali ya juu ya usafi.
Akifafanua aliongeza kusema kuwa katika jitihada za kuhakikisha zoezi la usafi katika manispaa hiyo unakuwa endelevu imejiwekea mikakati 16 ambapo imeainisha maeneo 24 ya kufanyiwa usafi.
“Baada ya agizo la Rais (Magufuli) manispaa hii imefanya mambo makubwa kwa kujiwekea mikakati 16 na katika mpango kazi wetu tumeainisha maeneo 24 ikiwa ni pamoja na kufanya usafi katika maeneo yaliyotengwa kwa shughuli za maziko ili kuhakisha zoezi hili la usafi linakuwa endelevu,” alisisitiza.
Alisema katika kutekeleza agizo hilo la Rais ambalo linafikia kilele chake leo, maofisa afya watafanya ukaguzi katika maeneo mbalimbali ikiwa pamoja na kutembelea nyumba kwa nyumba na watakaobainika kutitirisha maji machafu wataadhibiwa kwa kutozwa faini ya Sh 50,000.
“Zoezi hili la usafi pia limelenga kudhibiti mlipuko wa magonjwa ya kuhara ukiwemo kipindupindu. Pia tutahakikisha vyoo vyote ambavyo vimeshajaa vinanyonywa …tayari tumeshatoa elimu ya afya shuleni na kwa wananchi ikiwa ni kusimamia sheria mbalimbali za usafi wa mazingira na kuhakikisha zinatekelezwa,” alisema.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, Mkuu wa Shule ya Sekondari Kalangasa, Gabriel Hokororo amekiri kupokea agizo la Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga likiwataka kuwepo kazini leo na kila shule iwe imepanga na kuainisha maeneo ambayo yatafanyiwa usafi wa hali ya juu.
“Kwa shule za kutwa tumeagizwa wanafunzi nao wawepo shule ikiwa ni kutekeleza agizo la Rais (Magufuli) kwa kufanya usafi tena usafi wa hali ya juu ….. leo pamoja na kuweka mazingira ya shule katika hali ya usafi pia tutapanda aina mbalimbali za maua na miche ya miti mbalimbali,” alieleza
Chanzo: HabariLeo