Friday, January 1, 2016

Walanguzi wa Madini ya Tanzanite Wasakwa


Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Operesheni hiyo imeanzia katika Mji wa Mererani, wilayani Simanjiro kabla ya kuhamia maeneo mengine ya mikoa ya Arusha na Manyara.

Kamishna wa Madini Kanda ya Kaskazini, Alex Magayane alisema inafanyika kwa agizo la Serikali la kutaka kuona watu wanaofanya biashara hiyo wanafuata utaratibu ukiwamo kuwa na leseni.

“Mimi nipo likizo, lakini naitambua hiyo operesheni kuwa ni mkakati ambao tumepanga kudhibiti biashara holela ya madini hasa ya Tanzanite,” alisema Mgayane.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Madini Mkoa wa Manyara (Marema), Sadick Mnene alidai kuwa operesheni hiyo inafanyika kinyume na utaratibu.

Alisema baadhi ya wachimbaji wadogo wanavamiwa na kunyang’anywa mchanga wao wenye madini na haijulikani unapelekwa wapi. “Katika machimbo ya Tanzanite, kuna utaratibu wa kutolewa bure mchanga wenye chembe ndogo za madini kwa wajane na wenye shida ili wachekeche wajipatie fedha kidogo, lakini nao wanakamatwa na kunyang’anywa,” alidai.

Alisema hakuna anayepinga hatua hiyo, bali Serikali iwaeleze wale inaowatuma kufanya operesheni hiyo wafuate utaratibu na iwakamate wale wanaostahili waache kuwanyanyasa wasio walengwa.

Alishauri Wizara, Polisi na wachimbaji kufanya mazungumzo ya kutafuta njia mbadala ya kupunguza ada ya leseni inayochangia watu kufanya biashara kiujanjaujanja.

Alisema ada ya leseni ya madalali wazawa imepanda kutoka Sh120,000 hadi 250,000.

“Kuna madalali zaidi ya 5,000 Arusha na Mererani, sasa kama gharama ya leseni ingekuwa siyo kubwa, wengi wangelipa, sidhani kama wangeendelea kufanya kinyemela,” alisema Mnene.

Imeelezwa kuwa operesheni hiyo inafanyika baada ya Serikali kujikuta hainufaiki na madini ya Tanzanite ambayo hayapatikani duniani kote zaidi ya Tanzania pekee.