DEREVA wa bodaboda, Colnery Mpande (18), mkazi wa Kiluvya Kwa Komba,
amekufa baada ya pikipiki aliyokuwa akiiendesha kugonga gari kwa nyuma
na yeye kuangukia barabarani na kukanyagwa kichwa na gari lingine.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Bonaventura Mushongi alisema
pikipiki hiyo baada ya kuligonga gari hilo ilipoteza mwelekeo na
kuanguka barabarani kisha kugongwa kwa kukanyagwa kichwa na kufa papo
hapo.
Alisema tukio hilo ni la jana saa 10 alfajiri eneo la Mpakani, katika barabara ya Morogoro wilayani Kibaha.
Kamanda alisema gari aliloligonga kwa nyuma dereva huyo wa bodaboda
lilisimama ghafla na halikuonesha ishara kwamba linakatisha kuingia
kushoto.
Alisema Mpande alikuwa akiendesha pikipiki yenye namba za usajili MC
332 AXL aina ya Sanlg akitokea Kibaha kuelekea Kiluvya na aligonga gari
lenye namba za usajili T 616 DCB aina ya Mitsubishi Canter lililokuwa
likiendeshwa na Shaaban Ally kutoka Kibaha kwenda Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Kamanda, Mpande alikanyangwa kichwa na lori la mizigo
lenye tela na namba za usajili T 559 BFA/T 874 AQF likiendeshwa na
Daniel Joseph aliyekuwa akitokea Dar es Salaam kwenda Mbeya.
MATUKIO ZAIDI YA KUSISIMUA BOFYA HAPA>>