Thursday, March 17, 2016

Magufuli apiga simu kituo cha runinga na Kuchangia maoni yake

Rais wa Tanzania John Magufuli amewashangaza wengi baada ya kupiga simu katika kituo cha runinga asubuhi.

Rais huyo alipiga simu wakati wa kipindi cha Clouds 360 kueleza kufurahishwa kwake na kipindi hicho.
Tangu kuingia madarakani Novemba mwaka jana, kiongozi huyo hajafanya mahojiano yoyote ya moja kwa moja na kituo chochote cha habari.

“Mimi nawapongeza sana kwa kweli,” alisema Dkt Magufuli, kabla ya kuendelea na kutaja majina ya watangazaji wa kipindi hicho na kusema huwa wanachambua vyema magazeti.
Alisema aliwapigia simu kuwapongeza.
Mmoja wa watangazaji hao alichukua fursa hiyo kumuuliza swali Dkt Magufuli.

Swali lilihusu kutolewa kwa zawadi kwa wanawake lakini Dkt Magufuli alishangaa ni kwa nini hawakuwapa wanaume zawadi.

Baada ya kumaliza kuzungumza, Dkt Magufuli alimkabidhi simu mkewe Janet ambaye pia alieleza furaha yake kuhusu kipindi hicho.
“Yaani mnatupa faraja, huwa tunacheka sana na mzee wangu hapa,” alisema Bi Magufuli.

Baadaye alirejesha simu kwa Dkt Magufuli ambaye kwa utani aliwashauri watangazaji wakati mwingine wajitokeze na wachumba wao.

"Sam (Sasali) na mke wake, Babbie (Kabae) aje na mume wake na wewe Hudson (Kamoga) uje na mke wako hapo. Siku nyingine mwakaribishe hapo,” alisema.