MBUNGE wa Jimbo la Kigoma Mjini, Zitto Kabwe atafuta nafasi kukutana 
na Rais John Magufuli kumuomba atengue agizo la Rais Jakaya Kikwete la 
kuzuia ujenzi wa makazi katika Mlima wa Mlole Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Rais Kikwete alitoa agizo hilo mwaka 2006 kama moja ya hatua za 
kudhibiti mmomonyoko wa ardhi na kujaa mchanga kwa bandari ya Kigoma.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Kigoma 
Cinema mjini Kigoma, Mbunge huyo alisema ameamua kuchukua hatua hiyo kwa
 kuamini kwamba taarifa alizopewa Rais Kikwete zilizosababisha kutoa 
agizo hilo hazikuwa sahihi.
Zitto alisema Rais Kikwete alipewa taarifa potofu kwamba mmomonyoko 
wa udongo kutoka katika eneo hilo ndiyo unaosababisha kujaza mchanga na 
kupunguza kina katika bandari ya Kigoma.
Mbunge huyo wa Kigoma Mjini alisema kuwa tafiti zilizofanyika na 
taarifa zilizopo zinaonesha kuwa kupanuliwa kwa Mto Lukuga kunafanya 
maji kutoka kwa wingi na kuingia bahari ya Atlantiki ndiko kulikochangia
 kupunguza kina cha maji katika maeneo mbalimbali ya mwambao wa Ziwa 
Tanganyika.
Kwa mujibu wa tathmini iliyofanywa mwaka 2008 inaonyesha kuwa kiasi 
cha Sh bilioni tano kilikuwa kikihitajika kwa ajili ya kuwalipa fidia 
wakazi hao, fedha ambazo uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma 
Ujiji imesema haiwezi kuzilipa hivyo kutaka mamlaka za serikali kuona 
namna ya kutafuta fedha hizo na kugharamia kuwalipa watu hao.
Wakizungumzia kauli ya Zitto, baadhi ya wakazi wa eneo la Mlole ambao
 wameathirika kwa kiasi kikubwa na agizo hilo la Rais Kikwete, walisema 
kuwa wameanza kupata matumaini ya kuona thamani ya nyumba zao kwani 
tangu kutolewa kwa agizo hilo nyumba zao zimekuwa hazina thamani mahali 
popote.
