Saturday, April 16, 2016

Aliyemdhihaki Magufuli Mtandaoni Kizimbani

 
Mtuhumiwa Isaac Emire (katikati) akiongozwa na askari kuelekea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kujibu mashtaka ya kesi hiyo jana.

MKAZI wa Olasiti Jijini Arusha, Isaac Emily (40), amepandishwa kizimbani kwa kumtolea maneno ya dharau na kumdhihaki Rais John Magufuli katika mitandao ya kijamii. Alisomewa mashitaka jana na Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Gaudencia Masanja mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Arusha, Augustino Rwezile.

Katika mashitaka hayo, Emily amedaiwa kutenda kosa hilo Machi 17 mwaka huu kinyume na sheria ya mitandao namba 16 kifungu namba 14 ya mwaka 2014. Masanja alidai kuwa, siku hiyo mshitakiwa alisambaza ujumbe wa uongo katika mitandao ya kijamii wenye lengo la kumdharau, kumdhihaki na kumtolea maneno Rais Magufuli yenye lengo la kumdhalilisha.

Alidai kuwa ujumbe huo ulisomeka, ”Hizi ni siasa za maigizo halafu mnamfananisha huyu bwege na Nyerere wapi bwana.’’ Mshitakiwa huyo alikana kutenda kosa hilo ambapo Mwendesha Mashitaka aliomba Mahakama isitoe dhamana kwa mshitakiwa huyo, kwa maelezo kuwa ingawa dhamana ni haki yake ya msingi, lakini usalama wake utakuwa shakani kwani watu wengi wamekerwa na ujumbe huo na pia akiwa nje anaweza kuvuruga ushahidi.

Hata hivyo, Emily hakukubaliana na madai ya Mwendesha Mashitaka na kusema ana uhakika hataingilia upelelezi wa kesi hiyo kwa sababu simu zake zote ziko mikononi mwa Polisi, hivyo madai ya kusema ataingilia upelelezi si ya kweli. Mtuhumiwa pia alijitetea kuwa maisha yake yatakuwa salama endapo atapata dhamana, hivyo kuiomba mahakama impe dhamana.

Chanzo: HabariLeo