Monday, April 11, 2016

Seif ajisafisha kwa wana CUF

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Seif Sharif Hamad amesema uamuzi wa chama chake kususia uchaguzi wa marudio uliafikiwa na Baraza Kuu la Uongozi na hauna uhusiano na taarifa kwamba amenunuliwa na Chama Cha Mapinduzi pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Aidha Seif amelazimika kutolea ufafanuzi ukarimu aliofanyiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kumlipia safari ya matibabu kwenda India; Serikali ya Jamhuri ya Muungano kulipa gharama za kuwepo katika Hoteli ya Serena na kutembelewa na viongozi wa ngazi za juu akisema, havina uhusiano na kurubuniwa.
Katika kile kinachoonekana ni ‘kuwaangukia’ wanachama wake kupitia mkutano wa waandishi wa habari aliofanya jana mjini hapa, Seif alisema huo ni ukarimu na utamaduni wa viongozi unaotokana na ubinadamu .
Alisema uamuzi wa kujitoa katika uchaguzi wa marudio wa Machi 20 ulitokana na chama hicho kutokubaliana na uamuzi uliofikiwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kwa sababu uchaguzi huo ulikidhi mahitaji na matarajio ya wananchi CUF iwe madarakani.
Kwa mujibu wa mwanasiasa huyo aliyekuwa mgombea wa urais wa Zanzibar kupitia CUF, zipo taarifa kutoka kwa baadhi ya watu wanaodai kwamba alijitoa kwenye uchaguzi huo wa marudio baada ya kurubuniwa na CCM ili ipate ushindi mkubwa.
“Taarifa hizo hazina harufu ya ukweli,” alisema. “Kilichofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kugharimia safari yangu ya kwenda India matibabuni pamoja na kutembelewa na viongozi wa ngazi za juu akiwemo Rais John Magufuli , kwanza ni wajibu wa serikali kwa sababu mimi ni Makamo wa Kwanza wa Rais mstaafu….lakini huo ndio ukarimu na uhusiano wetu Watanzania unaotokana na ubinadamu,” alisema.
Alisema msimamo wa CUF kutoitambua Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya Rais Dk Ali Mohamed Shein, upo pale pale kwa sababu chama hicho kinaamini kilishinda katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 kwa kupata majimbo ya uchaguzi ya Unguja na Pemba.
“Chama cha CUF hakijabadili msimamo wa kutoitambua Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Rais Dk Ali Mohamed Shein kwani sisi tunaamini kwamba tulishinda katika uchaguzi wa Oktoba 25 kwa kupata ridhaa ya wananchi walio wengi ambao walikipigia kura chama chetu na kupata ushindi wa majimbo yaliyopo Unguja na Pemba,” alisema.
Juzi wakati Rais wa Zanzibar akizungumza na waandishi wa habari na kutangaza Baraza la Mawaziri, Ikulu, alisema ushindi wake unatambuliwa na wananchi walio wengi ambao ndiyo walioipa ridhaa CCM na kushika hatamu ya kuongoza dola kwa asilimia 91.4.