Saturday, April 9, 2016

Wabunge zaidi kizimbani kwa rushwa, Msekwa afunguka

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Mhandisi Felchesmi Mramba.

Siku chache baada ya wabunge wanne kupandishwa kizimbani wakituhumiwa kwa rushwa, gazeti hili limedokezwa kuwa, juma hili wabunge wengi zaidi watafikishwa mahakamani wakikabiliwa na tuhuma kama hizo.
 
Wabunge ambao tayari wamefikishwa mahakamani ni Mbunge wa Sumve (CCM), Richard Ndassa (56), akituhumiwa kuomba rushwa ya Sh milioni 30 kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Mhandisi Felchesmi Mramba.
Wengine ni Kangi Lugola wa Mwibara, Sadiq Murad wa Mvomero na Victor Mwambalaswa wa Lupa, wote wakiwa ni kutoka CCM.
 
Lugola, Murad na Mwambalaswa ambao ni wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (LAAC) walifikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuomba rushwa ya Sh. milioni 30 kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Gairo, Mbwana Magotta, ili wamsaidie kutoa mapendekezo mazuri ya taarifa ya hesabu za halmashauri hiyo za mwaka 2015/2016.
 
Mbali na wabunge hao, juma lililopita pia vigogo wengine walifikishwa mahakamani, Kamishina Mkuu wa zamani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya, aliyekuwa Ofisa Mwandamizi wa Benki ya Stanbic tawi la Tanzania, Shose Sinare na aliyekuwa Mwanasheria wa benki hiyo, Sioi Solomon.
 
Vigogo hao wanakabiliwa na mashitaka ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa dola milioni sita za Marekani sawa na zaidi ya Sh. bilioni 12 ambazo ni mali ya serikali ya Tanzania.
 
WABUNGE ZAIDI KIZIMBANI
Taarifa ambazo Chanzo chetu kimezipata, zinaeleza kuwa, juma hili wabunge wengi zaidi watapandishwa kizimbani kwa tuhuma za rushwa.
Taarifa hizo zinasema kuwa, kwa ujumla idadi ya wabunge watakaofikishwa makahamani kwa tuhuma hizo wanaweza kufikia 15, wengi wao wakiwa wameomba rushwa kupia kamati zao.
 
“Wote watapandishwa na Takukuru, hali hii imefanya wabunge waishi kwa mashaka sana, kuna wakati walikuwa wanataka kuitisha kikao cha wabunge wa CCM ili kujadili hali hii lakini naona mambo yameshindikana baada ya bwana mkubwa, (Rais John Magufuli) kupata taarifa na kuwa mkali,” alisema mmoja wa wabunge wa CCM.
 
Taarifa hizo zinadai pia kuwa, wabunge hao walikuwa na mpango wa kuchangia wenzao fedha za mawakili wanaosimamia kesi zao suala ambalo bado hawajaafikiana kutokana baadhi yao kupinga.
 
“Kwa kweli hii hali ya kamaka kamata siyo mzuri, inaharibu sifa yetu kama wabunge, nadhani ingetosha mamlaka za Bunge kushughulikia wale wanaotuhumiwa,” alisema Mbunge mwingine.
 
SAKATA LA STANBIC
Mbali na wabunge, inadaiwa wakati wowote Takukuru itawafikisha mahakamani vigogo wengine wanaokabiliwa na mashitaka ya mabilioni ya Uingereza na benki ya Stanbic Tanzania.
 
MSEKWA AFUNGUKA
Spika wa zamani wa Bunge la Tanzania na Katibu wa Baraza la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Pius Msekwa, amezungumzia kamata kamata hiyo ya  wabunge na kusema licha ya kufikishwa mahakamani wataweza kuendelea na uwakilishi wao wa wananchi mpaka pale mahakama itakapoona wana hatia.
 
Msekwa alisema hayo kutokana na gazeti hili kutaka kujua hatma ya wabunge hao kupitia uzoefu wake wa kuwa kiongozi wa Bunge.
"Hao wabunge wanaruhusiwa kuendelea na majukumu yao ya kibunge kwa sababu bado wanatuhumiwa tu na haijathibitika wametenda kosa. Katika mabunge yote ya Jumuiya ya Madola iwe Uingereza, Zambia au Singapore, sheria na taratibu zinafanana, kwa hiyo wakiwa ndani ya Bunge wanachangia tu  kwenye mijadala,  wanalindwa na sheria za Bunge," alisema Msekwa.
 
Kuhusu namna tuhuma hizo zilivyoibuka na maendeleo yake hadi sasa, Spika huyo wa zamani alisema Mbunge yeyote anapokuwa nje ya Bunge ni raia sawa na Watanzania wengine, hata kama anaweza kuwa machachari na mwenye hoja kali anaweza kutikiswa na tuhuma za namna hiyo.

Chanzo: Nipashe