Saturday, May 28, 2016

Mwenyekiti na Mtendaji wa kijiji Mbaroni kwa kutafuna zaidi ya milioni 12

Mwenyekiti na Afisa mtendaji wa kijiji cha Mkwajuni wilayani Songwe, wanashikiliwa na jeshi la polisi, baada ya wananchi kuwatuhumu kwa kutafuna zaidi ya shilingi milioni 12 mali ya kijiji hicho pamoja na kushindwa kusoma mapato na matumizi ya kijiji kwa zaidi ya miezi tisa.
Wananchi walionyesha furaha yao, wakishangilia hatua ya viongozi wao kupelekwa mahabusu baada ya kufanyika mkutano wa hadhara ambao wananchi hao waliutumia kuazimia viongozi hao wakamatwe kwa tuhuma za kufanya ufisadi wa zaidi ya shilingi milioni 12 za ushuru wa minara ya simu iliyopo kijijini hapo.
Wakiijitetea kwenye mkutano huo, Afisa mtendaji wa kijiji hicho Severio Malyagila amezikana tuhuma hizo, kwa madai kuwa fedha hizo zilitumika kwa idhini ya halmashauri ya kijiji 
Hata hivyo wananchi hao hawakuridhishwa na maelezo ya Afisa mtendaji, na baada ya mjadala mrefu ndipo mwenyekiti wa muda wa mkutano huo, akatoa azimio kwa niaba ya wananchi, maazimio ambayo jeshi la polisi likaanza kuyatekeleza papo hapo kwa kuwakamata watuhumiwa.