SERIKALI ya Marekani imetangaza kuwa itatoa dola za Marekani milioni
800 kwa Tanzania kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Uthibitisho wa kutolewa kwa msaada huo, umetangazwa na Balozi wa
Marekani nchini, Mark Childress aliyekutana na kufanya mazungumzo na
Rais John Magufuli katika Ikulu ya Dar es Salaam jana.
Balozi Childress alisema kutolewa kwa fedha hizo ni uthibitisho kuwa
kutotolewa kwa fedha za awamu ya pili ya Mradi wa Changamoto za Milenia
(MCC-2), hakujaondoa uhusiano na ushirikiano wa Tanzania na Marekani,
ikiwemo utoaji wa misaada ya maendeleo.
“Tumezungumza mambo kadhaa, na wiki hii Tanzania na Marekani kupitia
shirika letu la misaada la USAID tunatarajia kutiliana saini mkataba wa
zaidi ya dola milioni 400 kwa ajili ya mwaka ujao, pia tumezungumza kuwa
kutakuwa na dola milioni 800 zitakazotolewa na Marekani kwa ajili ya
miradi mbalimbali na hii haihusiani na MCC,” alisema Balozi Childress
muda mfupi baada ya kumaliza mazungumzo na Rais Magufuli.
“Ukweli ni kwamba tunayo mengi ya kufanya pamoja katika sekta
mbalimbali zikiwemo afya, elimu na kilimo na tutafanya kila juhudi
kuhakikisha haya yanafanikiwa,” alisema. Naye Rais Magufuli alisema
Serikali yake ya Awamu ya Tano, itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano
na ushirikiano na Marekani na kwamba fedha za msaada kutoka Marekani ni
muhimu kwa maendeleo ya Tanzania.
“Amekuja kutuhakikishia kwamba watatoa hela kwa ajili ya Tanzania na
anasema sasa hivi watatoa zaidi ya dola milioni 800, na mkataba mwingine
tunaweza tukasaini hata kesho wa dola milioni 410.
“Anasema kutotoa hela za MCC hakuna maana kupotea kwa urafiki wa
Tanzania na Marekani, urafiki wa Tanzania na Marekani upo pale pale na
sasa wanaongeza hela nyingi zaidi katika kuonesha kwamba juhudi za Hapa
Kazi Tu zinaendelea,” alisema Rais Magufuli.
Miezi michache iliyopita, Marekani ilitangaza kusitisha utoaji wa
fedha za miradi ya MCC- 2 ikitoa sababu mbili, ikiwamo kupitishwa kwa
Sheria ya Makosa ya Mitandao na Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli jana alikutana na Naibu Waziri
Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji, Didier Reynders na
kuzungumzia kuendeleza na kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo hususan
katika maendeleo.
Pamoja na kuzungumzia miradi ya ushirikiano inayotekelezwa kati
Tanzania na Ubelgiji katika mkoa wa Kigoma, viongozi hao pia
walikubaliana kuongeza ushirikiano katika biashara na uwekezaji, huku
Didier Reynders akiahidi kushawishi kampuni nyingi za Ubelgiji kuja
kuwekeza nchini.
Aidha, Rais Magufuli ameagana na Balozi wa Italia nchini, Luigi
Scotto aliyemaliza muda wake wa miaka mitatu. Wakati huo huo, Rais
Magufuli jana alitia saini kitabu cha maombolezo katika Ofisi ya Ubalozi
wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Nchi za Kiarabu ya Saharawi, Mikocheni
jijini Dar es Salaam kutokana na kifo cha Rais wa nchi hiyo, Mohamed
Abdelaziz aliyefariki dunia Jumanne iliyopita.
Rais Magufuli ambaye alipokelewa na Balozi wa Saharawi nchini, Brahim
Salem Buseif alisema Abdelaziz ambaye pia alikuwa Katibu Mkuu wa Chama
cha Polisalio Front, atakumbukwa kwa juhudi zake za kupigania ukombozi
na Uhuru wa Saharawi.
MATUKIO ZAIDI YA KUSISIMUA BOFYA HAPA>>