MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Iringa imemhukumu Johnface Lyang’oka ambaye
ni mkazi wa Magozi, Pawaga wilayani Iringa kifungo cha miaka 15 jela au
kulipa faini ya Sh bilioni 1.65. Amepewa adhabu hiyo baada ya kupatikana
na makosa mawili yaliyomhusisha na biashara ya meno ya tembo 34.
Lyang’oka alifikishwa mahakamani hapo pamoja na mtuhumiwa mwingine
katika kesi hiyo, Halfani Balobani baada ya kukamatwa Julai 30, 2015
akituhumiwa kutenda makosa hayo kati ya Julai 16 na 18, 2015.
Mahakama hiyo ilimuachia huru, Balobani aliyekuwa mshtakiwa wa kwanza
katika kesi hiyo iliyohusisha watuhumiwa wengine wanne, ambao
hawajakamatwa baada ya Lyang’oka aliyekuwa mshtakiwa wa pili kukana
kumfahamu mtuhumiwa namba moja katika kesi hiyo.
Akitoa hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Andrew Scout
alisema; “Mahakama imeridhishwa na ushahidi uliotolewa na mashahidi
wanne wa upande wa mashtaka dhidi ya washtakiwa hao.”
Alisema Mahakama imemuona Balobani hana hatia baada ya mshtakiwa
mwenza kukana kumfahamu na badala yake kuwataja watu wengine wanne ambao
hawakufikishwa mahakamani hapo kwakuwa hawajakamatwa na Polisi ili
waunganishwe katika kesi hiyo.
“Kwa hiyo Mahakama yangu imemtia hatiana kwa kuzingatia ushahidi
uliotolewa Johnface Lyang’oka na ninamhukumu kama ifuatavyo,” alisema.
Alisema katika shtaka la kwanza linalomhusisha Lyang’oka na biashara ya
meno ya tembo kinyume na Kifungu cha Sheria 80(1) na 84(1) ya Sheria ya
Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009 inayokwenda sambamba na Kifungu cha 14
(d) na Kifungu cha 57 cha Sheria ya Uhujumu Uchumi ya mwaka 2002
anahukumiwa: “Kwenda jela miaka 15 au faini ya Sh 1,548,000,000 baada ya
kuuza meno ya tembo 32 ambayo kwa wakati huo yalikuwa na thamani ya Sh
516,000,000,” alisema hakimu huyo.
Alisema katika shtaka la pili, mtuhumiwa katika kipindi hicho hicho,
alijihusisha na biashara ya meno ya tembo mawili ambayo wakati huo
yalikuwa na thamani ya Sh 32,250,000 kinyume na sheria hiyo.
Scout alisema kwa mujibu wa sheria hiyo ya wanyamapori, mtuhumiwa
akikutwa na hatia anatakiwa kulipa mara tatu ya thamani ya meno ya tembo
kwa wakati huo, hivyo kwa makosa hayo mawili Lyang’oka anatakiwa kulipa
faini ya Sh 1,644,750,000 au jela miaka 15.
MATUKIO ZAIDI YA KUSISIMUA BOFYA HAPA>>