Wednesday, June 15, 2016

Mwalimu mbaroni kwa kumpa mimba mwanafunzi

  
 Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Agrey Mwanri
Polisi wilaya ya Igunga mkoani Tabora wanamshikilia Mwalimu Edward Kashuma anayefundisha shule ya msingi Simbo, kwa tuhuma ya kumpa mimba mwanafunzi mwenye umri wa miaka 15 wa anayesoma kidato cha kwanza katika shule ya sekondari Simbo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora Kamishna Msaidizi, Hamisi Issa, alithibitisha kukamatwa kwa mwalimu huyo ambapo alidai upelelezi utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma inayomkabili.
Kutokana na tukio hilo, Issa amewaonya walimu na wananchi kuacha tabia ya kufanya mapenzi na wanafunzi na kukatisha masomo yao kwani kufanya hivyo ni kosa la jinai na ni kosa la ubakaji kwani wanafunzi wengi wako chini ya miaka 18.
Hata hivyo akizungumza kwa uchungu babu na mwanafunzi huyo Luteni Kanali mstaafu Thadeo Mgoso aliliambia gazeti hili kuwa yeye aliporudi nyumbani toka Dar es Salaam kuja kuhani msiba alikuta mjukuu wake haendi shuleni na alipomuuliza dada yake ambaye hakuweza kumtaja jina aliambiwa kuwa amefukuzwa shuleni kwa ajili ya ujauzito.
Baada ya majibu toka kwa dada yake aliamua kwenda shuleni kuonana na mwalimu mkuu wa shule hiyo ili kujua juu ya mjukuu wake kukatazwa kwenda shuleni hata hivyo aliambiwa mjukuu wake ni mjamzito na alipomuuliza mwanafunzi huyo alidai kuwa alipewa mimba hiyo na Mwalimu Edward Kashuma.
Kufuatia hali hiyo Mgoso alikwenda Kituo kidogo cha Polisi kutoa taarifa ili mwalimu aweze kukamatwa ambapo Mkuu wa Kituo cha Polisi Simbo, David Lukumay alimwambia atampigia simu ili aweze kuja kituoni lakini pamoja na kukaa muda mrefu kituoni hakuweza kufika.
“Kwa kweli huyo mkuu wa kituo ni mtu wa ajabu mpaka naondoka kituoni mshtakiwa hakuweza kufika pamoja na kupigiwa simu alisema babu wa mwanafunzi huyo. Sambamba na hayo Luteni Kanali Mgoso alibainisha kuwa kilichomshangaza yeye ni maelekezo aliyompa mkuu wa kituo, mtuhumiwa ya kutaka waelewane kwa kile alichodai mwalimu kuwa endapo atamfikisha kwenye vyombo vya sheria anaweza kufukuzwa kazi.
Babu huyo wa mwanafunzi alidai mwalimu huyo alifika nyumbani kwake akiomba waelewane na alipoulizwa juu ya mimba Mwalimu Edward Kashuma alikiri kufanya mapenzi na mwanafunzi huku akidai yeye alitembea naye mara moja mwaka jana mwezi wa kumi.
Aidha baada ya hali hiyo babu huyo alipiga simu Polisi tena na ndipo askari wawili walimfuata mtuhumiwa na kumuweka lupango ambapo amesema kesi hiyo atahakikisha anaifuatilia hadi mwisho pamoja na mkuu huyo wa kituo kutaka kuharibu kesi hiyo.
Naye Kaimu Mtendaji wa Kata ya Simbo, Felician Musiba amekiri mwalimu kukamatwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma ya kumpa mimba mwanafunzi wa kidato cha kwanza ambapo amewataka walimu kuacha tabia hiyo na badala yake wazingatie maadili ya kazi na kuacha vitendo vya kuidhalilisha taaluma ya ualimu.