Monday, June 13, 2016

Nyama ya ngo'mbe inayosadikiwa kuwa na Kimeta yasababisha vifo Dodoma.


Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana
WATU watatu wa familia moja wamefariki dunia mkoani hapa kwa kile kinachoelezwa ni kutokana na kula nyama ya ng’ombe aliyekuwa na ugonjwa wa kimeta. Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa amethibitisha tukio hilo na kusema marehemu hao ni wa kijiji cha Mwaekesabe, kata ya Kimaha wilayani Chemba.

Amewataja waliokufa kuwa ni Haji Nchalo (20) na watoto pacha, Yassir na Yassin wenye umri wa miaka saba wote wakazi wa kijiji cha Mwaekesabe. “Tunahisi walikula nyama yenye kimeta ila uchunguzi bado unaendelea, ukikamilika tutatoa majibu,” alisema.

Akielezea tukio hilo, baba mzazi wa marehemu hao, Salum Nchalo ambaye naye amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma akihisiwa kula nyama hiyo, alisema watu tisa walikula nyama hiyo, wakiwemo yeye, mkewe na watoto wao saba na watatu kati yao ndio waliofariki.

Alisema walikula nyama hiyo Jumamosi ya Mei 28 mwaka huu aliyopewa na jirani yake Bakari Juma mara baada ya ng’ombe wake kuumwa, hivyo kuamua kumchinja. “Nyama nilipewa na jirani yangu Bakari Juma ambaye alikuwa amewekeza ng’ombe kwa Iddi Kibure… Kibure alimletea ng’ombe huyo akidai anaumwa hivyo akaamua kumchinja na nyama kutupatia,” alisema.

Aliongeza kuwa, Juma aligawa nyama kwa kaya nane kijiji hapo, lakini akaelezea kushangazwa kuona ni familia yake pekee ndiyo iliyoathirika. Mganga wa zamu katika wodi namba 12 ilipolazwa familia ya Nchalo, Rose Msigwa alisema waliwapima vipimo vyote wagonjwa hao na hawakuona tatizo lolote.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Zainabu Chaula akizungumza kwa njia ya simu alisema kwa sasa yupo mbali na hospitali hawezi kuzungumza chochote.