Tuesday, August 30, 2016

Hivi Ndivyo Kupatwa Kwa Jua Kutakavyokuwa Kesho

Muonekano wa jua litakavyokuwa wakati wa kupatwa kwa jua.
KESHOKUTWA Septemba 1, 2016 litatokea tukio kubwa la angani ambapo kutakuwa na kupatwa kwa jua ambapo linatazamiwa kufanyika katika usawa wa anga ya Tanzania.
Tukio hilo linatazamiwa kuanzia saa 4:17 asubuhi hadi 7:56 adhuhuri siku hiyo.
Mashabiki na wanataaluma wa anga kutoka duniani kote pamoja na wanasayansi, wanafunzi pamoja na jamii ya Tanzania wataelekea Rujewa, kusini mwa Tanzania, karibu na Mbeya, kushuhudia duara la Jua linavyobadilika kuwa mithili ya pete.

Nchini kote Tanzania, siku hiyo mamilioni ya watu watashangaa kuona Jua kali la utosini likimegwa kwa zaidi ya asilimia 90 kwa kufunikwa na mwezi katika tukio hilo la kupatwa kwa jua. Hali hiyo italiacha jua lionekane kama pete au hilali nyembamba au mithili ya mwezi mwandamo.
Watu wanaoishi ndani ya ukanda wenye upana wa kilometa 100 unaokatisha kusini mwa Tanzania, kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuelekea Katavi, Mbeya, Ruvuma hadi Masasi na kuingia Msumbiji, siku hiyo wataona jua kama duara jembamba mithili ya pete, kwa vile asilimia 98 ya jua katika maeneo yao litakuwa limejificha nyuma ya mwezi. Kupatwa huko kwa jua kunaweza kuonekana kwa usalama na watazamaji, lakini inabidi kutumia vichuja maalum vya mwanga wa jua.
Tukio la kupatwa kwa jua ni la kusisimua na la nadra sana kutokea katika maisha ya mtu na baadhi ya dini kama Uislamu zinawataka watu wakati wa kipindi hicho kuwa kwenye swala maalumu. Vijana wengi katika kizazi hiki kipya watakuwa hawajaona tukio hili na hivyo ni tukio litakalowasisimua na wanafunzi ambao wamekuwa wakijifunza mashuleni watapata ushahidi wa moja kwa moia siku hiyo.

Wengine watazidi kujifunza sayansi ili kuelewa kwa nini kinatokea kile wanachokiona. Kwa hiyo tukio hili linaweza kutumiwa na shule na taasisi za elimu kuendeleza sayansi na kuvuta wanafunzi kujiendeleza kisayansi na hasa kuelewa mizunguko mbalimbali iliyopo katika mfumo wetu wa sayari pamoja na anga za juu kwa ujumla. Bila shaka wataongeza uelewa wa sayansi na umuhimu katika kuelewa maumbile ya ulimwengu wetu.
Kupatwa huku kwa jua kutatokea siku ya Alhamisi ambapo wanafunzi wengi watakuwa shuleni na litatokea wakati wa masomo. Kwa vile mchakato wote utaendelea kwa masaa manne hivi, kati ya saa 4:00 asubuhi hadi saa 8:00 mchana wanafunzi wataweza kushirikiana kuangalia, kusimulia na kujadili tukio ili kulielewa vizuri na kuandika ripoti madarasani mwao. Tukio jingine kubwa la kupatwa kwa Jua kama hili halitatokea miaka 15 ijayo, kwa hiyo tunahitaji kutumia fursa hii kwa ukamilifu kujifunza.
Ili kuangalia kupatwa huko, kila mmoja atahitaji kutumia kikinga macho kinachochuja mwanga wa Jua kiitwacho Kitazamia Jua. Nini hatari kuangalia jua lililopatwa kwa macho moja kwa moja au hata kutumia vichujio vingine vya kiza vilivyotengenezwa mitaani. Kitazamia Jua maalumu ni kifaa rahisi kilichotengenezwa kutokana na kichuja nguvu ya jua ambacho kinaondoa mionzi haribifu kwa asilimia 99.999.
Miwani hiyo maalumu ya Jua inaweza kutengenezwa Tanzania kwa gharama isiyozidi Sh 500 kila moja, ikiwemo kuchapa fremu za kadbodi na kichuja nguvu ya jua (polymer filter) kinachoagizwa kutoka Marekani.