Saturday, August 6, 2016

Inatisha: Bodaboda zaua watu 900

 
DAVID Nyamuhanga (20) amehitimu kidato cha nne mwaka jana na matokeo yake hayakuwa mazuri. Aliamua kuingia kwenye biashara ya kuendesha pikipiki ya biashara; maarufu kama bodaboda na ndipo alipoenda kwa rafiki yake akamfundishe jinsi ya kuendesha chombo hicho. Alifundishwa kwa siku tatu mfululizo.
"Nilipoona nimeweza, yule rafiki yangu alinipeleka kwa tajiri wake ili nikapewe pikipiki ya biashara. Bahati nzuri niliipata siku ile ile baada ya yule tajiri kuhakikishiwa na yule rafiki yangu kuwa mimi ni dereva mzuri," anasema Nyamuhanga.
Anaendelea kusema, "Kesho yake niliingia barabarani bila hata kuwa na leseni. Nilimwomba rafiki yangu anifanyie mpango wa leseni akanitaka nitafute Sh 50,000. Nilitafuta pesa hizo kwa ndugu zangu na bahati nzuri nikazipata. Kwa maelezo yake Nyamuhanga, hakupata mafunzo yoyote ya udereva.
Lakini tayari anayo leseni ya kuendesha pikipiki! "Nchi hii hakishindikani kitu, ni pesa yako tu. Kiukweli nimetumia njia ya mkato kupata leseni," Nyamuhanga anaeleza. Kijana huyo hana mafunzo. Lakini ana leseni ya udereva wa pikipiki na wala hasumbuliwi na polisi wa usalama barabarani. Kazi yake ni kubeba abiria na kuwapeleka maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam.
"Mara ya kwanza nilikuwa naogopa kuingia barabara za lami. Lakini siku hizi nimezoea tu na naenda sehemu yoyote ile," anaeleza Nyamuhanga akiwa amekwisha kufanya kazi hiyo kwa miezi sita sasa.
Nyamuhanga anawakilisha kundi la madereva wengi nchini ambao wameingia kwenye biashara ya pikipiki maarufu kama bodaboda bila kuwa na mafunzo.
Usafirishaji wa abiria kwa njia ya bodaboda katika Jiji la Dar es Salaam na kwingineko umegeuka kutoka huria kuwa holela tangu mwaka 2009 pale Serikali iliporasimisha usafiri wa pikipiki kama moja ya usafiri wa abiria nchini na fursa ya ajira kwa vijana.
Wakati ruhusa hiyo inatolewa hakukuwa na kanuni zilizoongoza usafiri huo na hivyo bodaboda waliokuwepo wakati huo waliendelea kutoa huduma hiyo bila kuwa na leseni ya usafirishaji abiria.
Hali kadhalika, kwa miaka mingi hakukuwa na chuo maalumu cha kutoa mafunzo ya udereva kwa waendesha pikipiki jambo ambalo lilifanya biashara hiyo kutokuwa na utaratibu unaoeleweka.
Hata vyuo ambavyo vilijitokeza kufundisha udereva vilikabiliwa na changamoto ya kutokuwepo kwa mtaala. Kutokana na hali hiyo, kumekuwepo na ongezeko kubwa la ajali za pikipiki na kufanya vijana wengi ambao wanajiingiza kwenye biashara hiyo kupoteza maisha na wengine kubaki na vilema vya kudumu.
Takwimu za Polisi Makao Makuu zinaonesha kwamba mwaka 2014 kulikuwa na ajali 4,169, vifo 923 na majeruhi 3,884 wakati 2015 pikipiki zilisababisha ajali 2,626, watu waliopoteza maisha walikuwa 934 na majeruhi 2,370.
Licha ya kwamba takwimu zinaonesha kwamba mwaka 2015 kulikuwa na upungufu wa ajali za pikipiki, kinyume chake kulikuwa na ongezeko la watu 11 waliopoteza maisha, lakini kukawa na upungufu wa watu 1,514 ambao walijeruhiwa.
Ofisa Uhusiano wa Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (MOI), Juma Almasi, anasema mwaka 2014 majeruhi wa pikipiki waliolazwa katika wodi hiyo walikuwa 941 na mwaka 2015 idadi ya majeruhi wa pikipiki iliongezeka na kufikia 1,013.
"Hii inaonesha kwamba idadi ya madereva wa pikipiki wanaopata ajali idadi yao inaendelea kuongezeka, hivyo Serikali na wadau wengine lazima wafanye jambo kuzuia kizazi hiki cha bodaboda kisiendelee kuangamia," anasema Almasi.
Moja ya sababu za ajali za pikipiki kuongezeka ni kutokana na wengi wa madereva wanaingia kwenye biashara hiyo bila kuwa na mafunzo yoyote ya udereva. Wengi hawajui alama za barabarani na wala hawajui sheria zinazowaongoza kufanya biashara hiyo. Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga, anasema asilimia 40 ya waendesha pikipiki hawana leseni.
Anasema kutokana na hali hiyo polisi kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali wameandaa mafunzo ya udereva kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini.
Kamanda Mpinga anakadiria kuwepo kwa madereva milioni moja nchini ambao wanafanya kazi ya kuendesha bodaboda. Lakini, nusu yao hawana leseni na wala hawana mafunzo yoyote ya udereva.
Kwa maelezo ya Kamanda Mpinga madereva wengi wanashindwa kuhudhuria mafunzo kutokana na tatizo la fedha za kulipia mafunzo na muda wa kuhudhuria mafunzo hayo.
Anazitaja baadhi ya taasisi ambazo ziko tayari kutoa elimu ya udereva na kuwafuata katika maeneo yao ni Chuo cha Future World, Chuo cha Usafirishaji (NIT) pamoja na Mamlaka ya Ufundi Stadi (Veta).
Mpinga anasema NIT kwa kushirikiana na taasisi na moja ya taasisi za nchini Uingereza wameandaa mtaala maalumu kwa ajili ya kuwafundisha masomo ya udereva waendesha pikipiki.
"Kupitia mfumo huo wa kuwafikia maeneo ya karibu na kuwapa elimu hiyo kwa muda wa wiki tatu, watapata elimu pamoja na kufanyiwa majaribio na kisha kupatiwa leseni na hivyo kupunguza wimbo wa madereva wasiokuwa na leseni," anasema Mpinga.
Peter Haule (35), ni dereva aliyepata leseni yake mwaka 2013 na anatoa huduma zake mjini Iringa. Anawataka Sumatra, Polisi, Manispaa na madereva wa bodaboda wakae kama timu ili kuona namna wanavyoweza kupata majibu ya changamoto za utekelezaji wa sheria za usafirishaji na Usalama Barabarani.
“Madereva wengi hawana mafunzo. Wengine zaidi wanaongezeka kila siku.Hilo linafahamika na watumiaji wengine wa barabara,” anasema Haule.
Daktari Bingwa wa Mifupa katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Dk Bryson Mcharo, anasema katika utafiti wake alioufanya kwa majeruhi 700 waliofikishwa hospitalini hapo kati ya mwezi Machi hadi Septemba mwaka 2011, alibaini kuwa nusu ya madereva waliokuwa wamelazwa hospitalini hapo hawakuwa na leseni za udereva.
"Unajua baada ya serikali kuruhusu biashara hii mwaka 2009, hakukuwa na msisitizo wa namna ya kuwapa mafunzo madereva hawa na hivyo wengi wanafanya biashara kiholela," anasema Dk Mcharo.
Matokeo yake vijana wengi walioingia kwenye biashara ya bodaboda wamebaki walemavu na wengine wamepoteza maisha. Anaongeza kuwa utafiti wake ulibaini kwamba madereva ambao hawaoni umuhimu wa helmeti ni wale ambao hawakuhudhuria mafunzo ya udereva vyuoni.
"Ukiangalia vijana wanaoletwa MOI wengi ni kati ya umri wa miaka 20 na 30. Hawa ndio waathirika wakubwa na ndio wengi wanaobaki vilema. Asilimia 5.5 ya majeruhi wanaofikishwa hapa MOI wanapoteza maisha," anafafanua Dk Mcharo.
Kwa mujibu wa Dk Mcharo kwenye utafiti huo, alibaini kuwa madereva wengine wa pikipiki wanakuwa na mafunzo yanayotolewa kienyeji huko mitaani.
"Nilibaini kuwa baadhi wanajifunza pikipiki kwa siku mbili na kuanza biashara ya kubeba abiria, hii ni hatari kubwa kwa maisha ya watu." Anasema mwendesha pikipiki anapopata ajali yuko hatarini kupoteza maisha kwa asilimia 21.
Kwa sababu hiyo, anashauri kuwa suala la mafunzo kwa madereva hao lizingatiwe kabla ya kupatiwa leseni.
Takwimu za utafiti wa Dk Mcharo alizozifanya wakati akifanya shahada yake ya uzamili katika taasisi hiyo kati ya Machi 15 na Septemba 15 mwaka 2011 unaonesha kwamba kati ya majeruhi 722, wenye elimu ya msingi walikuwa 472 (asilimia 65.4).
"Takwimu hizi zinaonesha kwamba madereva wengi wa bodaboda ni vijana ambao wamehitimu shule ya msingi na kuamua kuingia kwenye biashara hiyo," anasema Dk Mcharo.
Anabainisha kwamba watu wenye elimu ya sekondari walikuwa 177 (asilimia 24.5) wakati wale ambao hawakuwa na elimu ni 22 sawa na asilimia 3.
Mchanganuo wa takwimu hizo unaonesha kuwa madereva wa pikipiki waliofikishwa MOI katika kipindi hicho ni 335 sawa na asilimia 46.4, abiria ni 175 sawa na asilimia 24.2 na watembea kwa miguu ambao walijeruhiwa na pikipiki ndani ya hiyo miezi sita ni 212 sawa na asilimia 29.4.
"Takwimu hizo zinaonesha kati ya watu hao waliofikishwa MOI, majeruhi 581 sawa na asilimia 66.6 ya waathirika ni vijana wenye umri kati ya miaka 21 na 40. Hii ina maana kuwa ajali nyingi za pikipiki zinapotokea waathirika wengi ni vijana ambao ndio rika la kuzalisha mali," anasema Dk Mcharo. 
 Chanzo: HabariLeo