Sunday, August 7, 2016

Wazazi wamuua mtoto kwa kipigo

MWANAFUNZI aliyekuwa akisoma Darasa la Saba katika Shule ya Msingi Zimba, Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga, Susana Kauzeni (15) ameuawa baada ya kupigwa na wazazi wake wakimtuhumu kuwa ni mtoro sugu wa shule.

Ofisa Elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga (Shule za Msingi), Peter Fusi alilieleza gazeti hili ofisini kwake kuwa mwanafunzi huyo alizikwa kijijini humo Julai 23, mwaka huu.

“Baba na mama yake walichangia kumpiga binti yao huyo wakimtuhumu kuwa ni mtoro sugu wa shule pia nyumbani amekuwa haonekani. Baba yake mzazi amekimbia baada ya kufanya uhalifu huo huku mama yake akiwa ameshikiliwa na Jeshi la Polisi,” alieleza Fusi.

Fusi alieleza kuwa kuanzia Agosti 3 na 4, mwaka huu alitembelea baadhi ya shule za msingi zilizopo kwenye Bonde la Ziwa Rukwa ikiwemo Shule ya Msingi Zimba kufuatilia kazi ya utengenezaji wa madawati mapya kwa ajili ya shule za msingi pia kufuatilia takwimu sahihi za wanafunzi ili kubaini wanafunzi hewa.

“Nilipofika kwenye Shule ya msingi Zimba, Mratibu Elimu Kata, Daudi Moga na Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Fidelis Mwangurumba walithibitisha kutokea kwa mauaji hayo ya wanafunzi huyo,” alisema.

Kwa mujibu wa Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Mwangurumba, mwanafunzi huyo alikuwa ni miongoni mwa wanafunzi watoro sugu shuleni hapo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo.