Tuesday, January 10, 2017

Ajikuta Kizimbani kwa kumkashifu Rais Magufuli

MTUNZA bustani Maganga Masele (25) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam akikabiliwa na mashitaka ya kutoa lugha chafu dhidi ya Rais John Magufuli na Makamu wake Samia Suluhu Hassan.
Maganga alifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka na Wakili wa Serikali, Lucy Mallya mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Respicius Mwijage.
Lucy amedai kuwa, Desemba 12, mwaka jana katika eneo la Leaders club, Kinondoni Dar es Salaam, Masele alitoa lugha ya matusi dhidi ya Rais Magufuli pamoja na makamu wake, jambo ambalo lingeweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Baada ya kusomewa mashtaka, Masele alikana kutenda kosa hilo na kuiomba mahakama impe dhamana.
Hakimu Mwijage alimuachia kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kusaini hati ya Sh milioni tano, pamoja na kuwa na mdhamini mmoja mwenye barua ya utambulisho.
Upelelezi wa kesi hiyo, haujakamilika.
Chanzo: HABARI LEO