Sunday, January 8, 2017

Gari Lililokuwa na Bosi wa CCM pamoja na Waandishi Laparamia mti

 Kamanda wa polisi mkoa wa Katavi, Damas Nyanda
WAANDISHI wa habari, viongozi wa Chama cha Mapinduzi(CCM) akiwemo Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Katavi wamenusurika kifo, baada ya gari walilokuwa wakisafiria, kuacha njia kisha kuparamia mti msituni.


Ajali hiyo ilitokea wakati wakitoka kwenye uzinduzi wa kampeni ya uchaguzi mdogo wa udiwani katika Kata ya Kasansa wilayani Mlele.
Mashuhuda ajali hiyo, walidai ilitokea Januari 6 saa 3 usiku katika eneo la Sikitiko ndani Hifadhi ya Taifa ya Katavi katika barabara ya Mpanda mjini kwenda Mpimbwe wilayani Tanganyika.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Damasi Nyanda alisema kuwa ajali hiyo ilihusisha gari aina ya Toyota Land Cruiser, mali ya CCM wilaya ya Mpanda, namba T 604 TEU, iliyokuwa ikiendeshwa na Charles Emmanuel (54), mkazi wa Mtaa wa Makanyagioa Manispaa ya Mpanda .
Walionusurika kifo ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Katavi, Mselem Abdallah, Katibu Mwenezi wa Mkoa wa CCM, Joseph Makumbule na Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM ya Mkoa, Jeneroza Mmbamba.
Waandishi wa habari walionusurika kifo ni Ernest Kibada wa Adam TV na Walter Mguluchuma, ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Katavi.
Alipohojiwa, Mguluchuma alisema ajali hiyo ilitokea wakati wakitokea kwenye kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata ya Kasansa, ambapo CCM walizindua kampeni zao .
Uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata ya Kasansa, utafanyika kufuatia kifo cha Sissto Cherehani aliyekuwa diwani wa kata hiyo kwa tiketi ya CCM. Uchaguzi huo utafanyika Januari 22 , mwaka huu.
Naye Kibada alisema kuwa dereva wa gari hilo, alishindwa kulimudu baada ya usukani wa gari hilo kukatika, hivyo liliacha njia na kuingia msituni kisha kuparamia mti. Alisema kuwa askari wa hifadhi ya taifa ya Katavi, walifika eneo hilo la tukio baada ya kupita saa mbili na kutoa msaada wa usafiri .
Chanzo: HABARI LEO