Wednesday, June 24, 2015

Kisa deni la Tambwe Mavungo azuiwa kuja Dar

Wakati wapenzi na mashabiki wa Simba wakiwa wamekaa tayari kumpokea mshambuliaji wao mpya Mrundi, Laudit Mavugo, imevuja kuwa deni la milioni 20 wanalodaiwa Wekundu hao wa Msimbazi, linaweza kufuta ndoto zao za kumpata nyota huyo.


Mshambuliaji wao mpya wa Simba Mrundi, Laudit Mavugo.
Simba wanadaiwa fedha hizo na Klabu ya Vital’O ya Burundi zikiwa ni gharama za uhamisho wa Warundi wawili waliowahi kusajiliwa na timu hiyo misimu miwili iliyopita ambao ni Amissi Tambwe na Gilbert Kaze.
Habari za kuaminika kutoka Vital’O ambazo Championi Jumatano limezipata, zimedai kuwa uongozi wa klabu hiyo umeitaka Simba ilipe kwanza fedha hizo ndipo iweze kumruhusu mchezaji huyo kujiunga na mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu Bara.
“Mavugo yupo tayari kuja kuitumikia Simba lakini uongozi umegoma kumruhusu kujiunga na timu hiyo kutokana na kuidai klabu hiyo kiasi cha dola 10,000 ambazo ni zaidi ya shilingi milioni 20 za Kitanzania.
“Fedha hizo ni zile ambazo Simba ilitakiwa kuzilipa wakati ilipowasajili Tambwe na Kaze misimu miwili iliyopita ambazo mpaka sasa hazijalipwa, hivyo uongozi imebidi umzuiye Mavugo kutua Simba mpaka hapo watakapokuwa wamelipwa deni hilo,” kilisema chanzo hicho cha kuaminika.
Hata hivyo, alipotafutwa Rais wa Simba, Evans Aveva simu yake iliita tu bila ya kupokelewa.
Na hata alipotafutwa msemeji wa timu hiyo, Haji Manara simu yake ya mkononi ilikuwa haipatikani.
Kuhusiana na hilo, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, Collins Frisch aliyesafiri hadi Burundi kushughulikia suala la Mavugo, alisema kweli Simba inadaiwa.
“Ni kweli, tunadaiwa dola elfu tano za zamani. Hilo tumelikubali na tuko kwenye mchakato wa kumalizana na Vital’O. Lakini si kweli kwamba wameweka masharti kwamba Mavugo hawezi kuja hadi hapo tutakapowalipa.
“Kaze yeye pia aliomba Vital’O wamsaidie kutudai, lakini rekodi zetu zinaonyesha ameshalipwa. Hivyo hatuna deni naye. Tena hata suala la Mavugo bado hatujafikia mwafaka hivyo hawawezi kuzuia kama ulivyosikia,” alisema Frisch.