Friday, August 14, 2015

Kiwanda Chafungwa Dodoma kwa Kusindika nyama za Punda...BOFYA HAPA=>

Baraza la taifa la usimamizi wa mazingira (NEMC) limekifungia kiwanda cha Huwa Cheng Company limited kilichopo mjini Dodoma na kutoza faini ya shilingi milioni 200 baada ya kubaini kiwanda hicho kinajihusisha na usindikaji wa nyama ya Punda kinyume na utamaduni wa watanzania huku mazingira yake yakiwa hatarishi kutokana na uchafu unaozalishwa kuzagaa kwenye makazi ya watu.

Ni mabishano makali baina ya wamiliki wa kiwanda hiki raia wa uchina na maofisa wa NEMC yaliyochukua muda mrefu kabla ya maofisa hao kutoa tamko la kufungwa kwa kiwanda hicho ambacho mbali na kuzalisha nyama ya Punda ambayo ni kinyume na utamaduni wa watanzania lakini pia mazingira ya uzalishaji wake ni hatarishi kwa afya za wafanyakazi na majirani wa eneo hilo.

Kiwanda hiki ambacho kwa siku kinadaiwa kuchinja Punda wasiopungua 200 inaelezwa kuwa mbali na kukiuka utamaduni lakini pia kinaharibu kizazi cha wanyama hao ambao uzao wake unatajwa kuwa ni mdogo hali inayotishia wanyama hao ambao kwa kanda ya kati hutumiwa katika kazi mbalimbali kupungua ama kutoweka kabisa. 
Mohamed Hamis ni meneja msaidizi wa kiwanda hiki ambaye anazungumza kwa niaba ya raia hao wa uchina anasema nyama hizo za Punda zinasafirishwa kwenda kuuzwa nchini China.

Sintofamahu hii inakifanya Chanzo chetu kuzungumza na wakazi wa mji wa Dodoma ambao wanatupa lawama kwa mamlaka za mkoa kutobaini kiwanda hicho na kukichukulia hatua huku kukiwa na taarifa ya nyama hizo kuzagaa na kuuzwa katika maeneo mbalimbali ya mji huo hasa kwenye mabaa na migahawa ya chakula.
Chanzo ITV