Kamanda wa Polisi mkoani
Kilimanjaro, Fulgence Ngonyani, aliiambia Nipashe jana kwa njia ya simu kwamba,
mgombea huyo alikuwa amekwenda kwenye klabu hiyo kwa ajili ya starehe na wakati
akiwa ndani alifuatwa na mmoja wa wateja wa klabu hiyo aliyejitambulisha
kwa jina la Oscar ambaye alimweleza kuwa ameegesha gari lake vibaya na kuzuia
magari mengine kutoka, jambo lililomuudhi. Ni kweli tukio hilo limetokea juzi
saa 7:00 usiku katika klabu maarufu ya Pub Alberto, na huyo Innocent
aliisalimisha bastola yake kituo kikuu cha polisi mjini Moshi, baada ya
kufikishwa hapo.
Tumewahoji na tumewaachia
kwa masharti ili kupisha uchunguzi zaidi, alisema Kamanda Ngonyani. Alisema,
Innocent alipohojiwa na polisi kuhusu madai hayo, alidai kupigwa na kuumizwa
sehemu ya jicho lake na hivyo alipatiwa fomu namba tatu ya matibabu (PF3) na
kwenda kutibiwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Kilimanjaro (Mawenzi).
Wakati mgombea huyo akidai kupigwa, mlalamikaji alidai kutishiwa kwa silaha na
Innocent baada ya kumtaka akaliondoe gari lake ili apishe gari jingine
lililokuwa likitaka kuondola eneo hilo.
Chanzo: Nipashe