Wednesday, October 14, 2015

Mwanaume Ahuhukumiwa Kucharazwa Viboko 360. HABARI ZAIDI BOFYA HAPA=>

Mzee mmoja kutoka Uingereza aliyepatikana na mvinyo nchini Arabia huenda akacharazwa viboko 360 kwa kosa hilo. Familia yake inasema huenda akafariki iwapo atapigwa viboko hivyo.

Karl Andree, 74, tayari amekaa mwaka mmoja gerezani tangu akamatwe na polisi wa kidini wa Saudia. Alikuwa amehukumiwa kufungwa jela mwaka mmoja na kuchapwa viboko 360.
Binti yake Kirsten Piroth amesema kwamba babake anaugua saratani na mwili wake hauna nguvu ya kuhimili viboko hivyo.
Pombe ni haramu kwa waislam na nchini Saudi Arabia na Bi Piroth anasema babake alikuwa akisafirisha pombe ya kujitengenezea kwenye gari lake Agosti 2014 alipokamatwa.
Bw Andree anakaribia kumaliza kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela na Bi Piroth anasema familia yake ilikuwa imeshawishika kuamini kwamba hangepigwa viboko hivyo kutokana na umri na afya yake.
Lakini anasema sasa hali imebadilika na huenda adhabu hiyo ikatekelezwa.
Wizara ya Mashauri ya Kigeni imesema inafuatilia kisa hicho.
Kwenye tovuti yake, wizara hiyo huonya kuwa adhabu ya kupatikana na pombe Saudi Arabia huwa “kali”.
Aidha, hutahadharisha wanawake dhidi ya kuendesha magari, uzinifu, ubasha na ulanguzi wa dawa za kulevya.
Adhabu ya ulanguzi wa dawa za kulevya Saudi Arabia huwa kifo.

Afisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron imesema ataiandikia barua Saudia Arabia kuhusu kumtambua msaamaha juu ya kisa hicho.