Sunday, October 25, 2015

Tume Ya Taifa Ya Uchaguzi Kutangaza Matokeo ya uchaguzi ndani ya saa 24. HABARI KAMILI GUSA HAPA>>

Tume ya taifa ya uchaguzi (Nec), imeahidi kutangaza matokeo ya uchaguzi wa madiwani na wabunge ndani ya saa 24 wakati yale ya Rais yatatolewa siku tatu baada ya kupiga kura.


Aidha Nec imewaagiza wasimamizi wa uchaguzi kwenye vituo kutotangaza matokeo ya ubunge na madiwani ndani ya muda huo.



Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damain Lubuva, aliwaambia wanahabari jana jijini Dar es Salam wakati akizungumzia upigaji kura wakati wa uchaguzi mkuu unaofanyika leo.



Alieleza kuwa matokeo ya awali ya urais yatatangazwa kwa hatua kadri tume itakavyokuwa inayapokea kutoka ngazi za chini.



Jaji Lubuva alisema Nec itajumlisha matokeo ya uchaguzi wa rais wa majimbo yote kwa nchi nzima na kumtangaza mshindi. 



Aidha aliwaambia mawakala wa vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi wa rais kuwa wanaruhusiwa kuwepo wakati wa kujumlisha matokeo ya kura hizo.



“Ni Nec pekee yenye mamlaka kisheria ya kumtangaza mshindi wa urais. Matokeo yatakayotolewa na tume ndiyo yanayoheshimiwa,” alisisitiza.



Aliwaambia wana habari kuwa mwaka huu wapiga kura milioni 23.25 waliandikishwa na kwamba jumla ya vituo 64,736 vitatumiwa kupiga kura Tanzania Bara ina vituo 63,156 na Zanzibar ni vituo 1,580, kwa mujibu wa maelezo yake.



Aidha alisema vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa 1:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni. Iwapo wakati wa kufunga kituo wananchi watakuwa kwenye mistari lakini ambao walifika kabla ya wakati wa kufunga kituo wataruhusiwa kupiga kura. 



Alisema baada ya kufika saa 10:00 jioni atakayefika baada ya muda huo hataruhusiwa.



Jaji Lubuva alivitaka vyama vya siasa vinavyoshiriki katika uchaguzi kuhakikisha kwamba vinaweka mawakala katika vituo vyote vya kupigia kura na kushiriki kujumlisha kura na kuwataka kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.



“Baada ya kupiga kura na kwa kuzingatia maadili ya uchaguzi ya 2015 yaliyokubaliwa na vyama vyote vya siasa na kuridhiwa na mahakama, wapiga kura wanatakiwa kuondoka vituoni na kuendelea na shughuli zao,” alisisitiza.



Alisema Tume inawahakikishia wananchi kuwa kutakuwa na ulinzi wa kutosha katika vituo vya kupigia kura.



“Tunatumaini kuwa amani na utulivu iliyokuwepo hadi itaendelea kama ilivyokuwa katika chaguzi zilizopita  ili kuhakikisha kwamba uchaguzi unafanyika kwa utulivu na amani kwa ustawi wa taifa letu,” alisema



Wakati huo huo , Chama cha Wamiliki wa Mabasi (Taboa) kimesitisha safari za mikoani ili kutoa nafasi kwa madereva pamoja na makonda kupiga kura kwani ni haki yao kikatiba. 
Chanzo: Nipashe

MATUKIO ZAIDI BOFYA HAPA=>