Monday, October 5, 2015

Wagombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) na wa umoja wa katiba ya Wananchi (Ukawa) kupitia Chadema, Edward Lowasa, wamegongana mkoani Manyara, mmoja akifanya kampeni zake Babati Mjini na mwingine Babati Vijiji, na kuvutia umati mkubwa wa wananchi.

LOWASSA
Akiwa Babati Vijijini jana, Lowassa aliwaahidi wananchi wa jimbo hilo kuwatatulia migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji iwapo atachaguliwa Rais wa Tanzania kupitia uchaguzi mkuu Oktoba 25, mwaka huu.

Aidha, aliwaahidi wakulima kuwatafutia soko la mchele ili wawe huru kuuza mazao yao sehemu yoyote ndani na nje ya nchi.

Alisema hayo mjini Magugu alipokuwa akizungumza na wananchi na kuaihidi kuwa akichaguliwa kuwa Rais ataunda tume ya maridhiano kwa ajili ya kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji.

"Migogoro ya ardhi inaniudhi sana na inanichosha sana lazima nitaitafutia ufumbuzi," alisema.

Alisema tume hiyo itakuwa kwa ajili ya kuangalia ni nani atakua amejipatia ardhi kwa dhuluma ili anyang'anywe.

Kuhusu wakulima wanaouza mchele, alisema atawatafutia soko kwa ajili ya zao lao hilo na kwamba ataanzisha kodi ambazo zitakuwa rafiki kwa wafanyabiashara ili waweze kuzimudu.

Akizungumzia elimu, Lowassa alisema kipaumbele chake cha kwanza ni elimu kwa sababu dunia imebadilika na hali ya elimu ya Tanzania ni duni.

"Hali ya elimu yetu ni duni sana, darasa la saba ni tabu, kidato cha nne ni tabu hadi chuo kikuu ni tabu na hadi wamelazimika kuweka alama za  kutunga," alisema.

Alisema katika serikali yake wanafunzi watasoma bure kuanzia darasa la kwanza hadi chuo kikuu.

“Hili litawezekana kwa kuuza magari ya   kifahari ya serikali aina ya shangingi na mapato ya gesi asilia,” alisema.

“Watu wananiuliza kuwa elimu itakuwaje bure wakati hakuna fedha?, yaani magari aina ya shangingi yote haya ya serikali yamejaa na gesi asilia kwa nini wanafunzi washindwe kusoma bure?...ni lazima tuwekeze kwenye elimu,” alisema. 

SUMAYE
Kwa upande wake, aliyekuwa Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, ambaye ni kiongozi wa kampeni za mgombea huyo urais wa Ukawa aliwataka wananchi kuwahi katika vituo vya kupigia kura asubuhi na mapema Oktoba 25, mwaka huu, kwa kile alichodai kuna mchezo 'mchafu' umeandaliwa kwa watakaochelewa  kupiga kura.

“Ujanja  unaweza kufanyika kwa wale watakaochelewa kufika vituoni wasiweze kupiga kura. Oktoba 25, mwaka huu kuna kazi ya kupiga kura kwa sababu tunaweza tukapiga kelele juu ya mabadiliko lakini kama hatutaenda kupiga kura itakuwa ni kazi bure," alisema.

Aidha, aliwataka wananchi kuwa makini wanapopiga kura ili wasiharibu kura zao.

Alisema katika karatasi za kupigia kura hakuna chama kinachoitwa Ukawa, hivyo wanatakiwa kuwa makini na wasome kabla ya kupiga kura.

"Kwenye zile karatasi za kupigia kura kuna chama kinaitwa Chadema, NLD, CUF na NCCR Mageuzi, hivyo unatakiwa kuweka tiki kwenye chama kimoja wapo ambacho kinaunda Ukawa," alisema na kuongeza:

"Utakapokuwa unaweka tiki, hakikisha hugusi kwenye boksi la mtu mwingine kwa sababu kwa kufanya hivyo utaharibu kura."

MAGUFULI
Naye mgombea urais wa CCM, Dk. Magufuli, akizungumza katika mkutano wa kampeni Babati Mjini jana, alisema Watanzania maskini wananyanyasika kwa kutozwa michango na ushuru wa aina mbalimbali, hivyo akiingia Ikulu atafuta michango hiyo ili nao waishi maisha bora kama walivyo wengine.

Aidha, alisema ataunda serikali itakayokuwa inatoa huduma za papo kwa papo kwa wananchi bila ya urasmu na kwamba hatavumilia utaratibu wa ovyo wa njoo kesho na michakato isiyo na mwisho.

“Imekuwa kawaida kuona Watanzania wa chini wakikandamizwa kwa  kutozwa ushuru usio wa lazima ambao mwingi unaishia kwenye matumbo ya watu wachache. Naomba urais ili nikawatumikie Watanzania wanyonge ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakinyanyasika ndani ya nchi yao kwa kukosa huduma mbalimbali ambazo hudaiwa fedha,” alisema.

Mgombea urais huyo wa CCM, alisema imekuwa kawaida kwa mwananchi wa kawaida kuombwa rushwa anapokwenda kutaka huduma mbalimbali, hivyo anaomba urais ili akomeshe vitendo vya aina hiyo.

“Nipeni urais muone nitakavyofunga mianya ya rushwa na ushuru usio na maana, mwananchi akiwa na nyanya zake ushuru, akienda kuuza vitumbua vyake ushuru, akiwa na kambuzi kake anapeleka mnadani ushuru, mimi John Magufuli nataka kwenda kufuta viushuru ushuru kama hivyo,” alisema na kuongeza:

“Nitawatumikia Watanzania wote bila kujali vyama vya siasa, hivyo nawaomba watu wa  vyama vyote mniunge mkono kwa kunipa kura nyingi zaidi ya aslimia 99 niwe Rais kwani nina nia ya dhati ya kuleta Tanzania mpya.”

“Naomba mniamini niko kwa ajili yenu na kwa ajili ya maendeleo ya Tanzania, nitawatumikia wote bila kujali tofauti zenu,  nipeni urais muone nitakavyopambana na ufisadi na wezi wa fedha za umma.” 

WALIOJENGA BARABARANI KUBOMOLEWA
Awali akiwa wilaya mpya ya Chemba, mkoani Dodoma, Dk. Magufuli alisema ingawa anaomba kura kuwania urais lakini watu waliojenga ndani ya hifadhi ya barabara watabomolewa bila kulipwa fidia kwasababu wamekiuka sheria za nchi ambazo ataapa kuzilinda akichaguliwa kuwa Rais.

Alisema hayo baada ya kuona mabango ya wananchi waliokuwa wanadai fidia. Wananchi hao ni waliobomolewa kupisha barabara ya kutoka Kondoa kwenda Dodoma ambao nyumba zao zilikuwa ndani ya hifadhi ya barabara.

“Ingawa anaomba kura lakini siwezi kuwadanganya wananchi waliojenga ndani ya hifadhi ya barabara kwamba watalipwa fidia. Kura nazihitaji sana lakini wale waliojenga ndani ya hifadhi ya barabara hawatalipwa fidia kwani ni kinyume cha sheria, maana fedha hizo bora zitumike kujenga barabara nyingine maeneo mbalimbali kuliko kulipa wavamizi wa barabara,” alisema.

Hata hivyo, aliwahakikishia waliojenga nje ya hifadhi ya barabara kwamba wasiwe na wasiwasi kwani serikali yake itawalipa fidia kwani barabara ndiyo imefuata makazi yao.

Alisema halmashauri zinapochukua ardhi ya wananchi kwa ajili ya matumizi mbalimbali zinapaswa kuwalipa fidia tena watakayokubaliana nayo.

Alisema sheria inazitaka halmashauri pia  kuwalipa wananchi mazao mbalimbali wanayoyakuta kwenye maeneo wanayotaka kuyatwaa kwa kazi za serikali.
 Chanzo: Nipashe