Tuesday, November 17, 2015

Wanafunzi Wanne Wafamaji mkoani Tanga

Wanafunzi wa shule ya msingi Lukole iliyopo kata ya Negero tarafa ya Kimbe wilayani Kilindi wamekufa baada ya kusombwa na maji ya mvua wakati walipokuwa wakijaribu kuvuka ng'ambo ya pili kwa kuogelea ndipo walipozidiwa na hatimaye kufa maji.

Akielezea tukio hilo, kamanda wa polisi mkoani Tanga kamishna msaidizi wa jeshi hilo Zubeir Mwombeji amesema limetokea katika kijiji cha Lukole kilichopo kata ya Negero wilayani Kilindi ambapo wanafunzi hao jamii ya wafugaji walikuwa na mifugo ndipo waliposhawishiana kuvua nguo zao ili waweze kuogelea hadi ngambo ya pili ndipo walipozidiwa hadi kufa maji.
Katika hatua nyingine, watu watatu wakazi wa jiji la Tanga na Dar es Salaam, wametiwa mbaroni na jeshi la polisi baada ya kupatikana na shehena ya dawa za kulevya aina ya Mirungi zaidi ya kilo 530 ambazo zilikuwa zikitokea nchi jirani ya Kenya kwenda jijini Tanga kwa ajili ya kusambazwa kwa mawakala wa biashara hiyo.

Kamanda wa polisi mkoani Tanga kamishna msaidizi wa jeshi hilo Zubeir Mwombeji amewataja watuhumiwa kuwa ni Mohamed Omary mkazi wa barabara ya 14 jijini Tanga, Haruna Hamis mkazi wa Tamta jijini Tanga na Aziz Athuman mkazi wa Dar es Salaam ambao wote kwa pamoja wamekamatwa katika eneo la mpirani lililopo kata ya chongoleani, tarafa ya chumbageni jijini Tanga.

CHANZO: ITV