Thursday, November 19, 2015

Wasifu Wa Majaaliwa, waziri Mkuu wa Tanzania

Bwana majaaliwa Kassim Majaaliwa, ambaye ameidhinishwa na Bunge kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, alizaliwa tarehe 22 Desemba mwaka 1960 yaani miaka 55 iliyopita.
Kitaaluma ni Mwalimu aliyepata elimu yake ya Ualimu katika chuo cha ualimu cha Mtwara mwaka 1991–1993.
Akitokea katika ukuu wa wilaya alioupata mwaka 2006 alijiunga na bunge mwaka 2010 alipogombea na kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Ruangwa mkoani Lindi.
Baadaye aliteuliwa kuwa naibu waziri wa tawala za mikoa na serikali za mitaa ofisi ya waziri mkuu wakati wa serikali ya awamu ya nne.
Bw Majaliwa ameidhiniswa kuwa Waziri Mkuu baada ya jina lake kuwasilishwa bungeni na Rais wa awamu ya tano wa Tanzania John Pombe Magufuli.
Amepigiwa kura na wabunge 258 kati ya 351 walioshiriki, ikiwa na maana kwamba amepitishwa na asilimia 73.5 ya wabunge.
Majaliwa Kassim anatokea kusini mwa Tanzania eneo ambalo mtu wa mwisho kutoka ukanda huo kuwa waziri mkuu alikuwa Mzee Rashid Kawawa aliyekuwa Waziri Mkuu miaka ya mwanzoni ya uhuru.
Waziri mkuu huyu mpya anakuwa mtu wa 11 kuwa Waziri Mkuu tangu Tanganyika ilipopata uhuru ambapo Waziri Mkuu wa Kwanza alikuwa Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Mawaziri wakuu wawili kati ya watangulizi wake wamehamia katika vyama vya upinzani


Jimbo la Ruangwa linapatikana Kusini Mashariki mwa Tanzania
Waziri Mkuu kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania atakuwa na madaraka juu ya udhibiti, usimamiaji, utekelezaji wa kila siku wa kazi na shughuli za Serikali, atakuwa na madaraka ya kuongoza shughuli za serikali Bungeni.

Atakuwa na madaraka ya kutekeleza au kusababisha utekelezaji wa jambo lolote au mambo yoyote ambayo rais ataagiza yatekelezwe.
Pia Waziri Mkuu atakuwa na madaraka ya kumshauri rais kuhusu uteuzi wa Mawaziri.
Anayo madaraka ya kumshauri rais kuhusu uteuzi wa wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri.
Waziri Mkuu huyu ni mpenzi wa mchezo wa mpira wa miguu na kwa kipindi kilichopita alikuwa Kocha wa timu ya soka inayoundwa na wabunge.