Saturday, December 26, 2015

Mapato Ya Gesi Sasa Hadharani

WAKATI eneo la kujenga kiwanda cha kuchakata gesi itakayovunwa baharini likitangazwa kupatikana wiki hii, uvunaji utakapoanza Serikali itapata mapato makubwa kutokana na mikataba minono iliyoingiwa.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili wiki hii, Mkurugenzi wa Utafutaji na Uendelezaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Kelvin Komba, amesema mfumo wa sasa wa mikataba, unaihakikishia Serikali kupata mpaka asilimia 85 ya faida yote ya kitalu, baada ya kutoa gharama za uzalishaji na ukataji kodi. Kwa mujibu wa Komba, mwekezaji akigundua gesi au mafuta, anatakiwa kurudisha gharama zake zilizotumika katika utafiti na baada ya hapo, faida hugawanywa kati ya Taifa na mwekezaji.
Taarifa zinaonesha kuwa mpaka sasa Tanzania kumefanyika ugunduzi wa gesi asilia katika eneo la bahari na nchi kavu, inayofikia takribani futi za ujazo trilioni 55.21. “Hata hivyo utajiri huu ili uwe na tija kwa Taifa ni lazima sheria, kanuni, sera na mikataba iwekwe katika namna ambayo inanufaisha Taifa,” alisema Komba.
Mgawanyo Akifafanua zaidi, Komba amesema Tanzania kwa sasa inatumia mfumo wa Mkataba wa Ugawanaji Mapato (Production Sharing Agreement-PSA), kati ya Taifa na mwekezaji, ambao mgawanyo wa mapato umewekwa kwa asilimia na hutofautiana kulingana na kiwango cha uzalishaji na maeneo ugunduzi ulipofanyika. Kwa mujibu wa Komba, kama ugunduzi ni wa nchi kavu, basi Serikali itapata asilimia 70 hadi 85 ya faida baada ya kodi kwa mafuta na asilimia 60 hadi 80 ya faida hiyo kwa gesi asilia.
Kama ugunduzi umefanyika katika kina kirefu cha bahari, Komba alisema mgawanyo unakuwa asilimia 60 hadi 85 ya faida baada ya kodi, ambao huongezeka kwa upande wa Serikali kadri uzalishaji unavyoongezeka. Kwa maana hiyo, mwekezaji baada ya kufanya utafiti, kugundua gesi au mafuta, akianza kuzalisha tu na kurejesha gharama za utafiti, katika faida baada ya kodi ataambulia kati ya asilimia 40, kiwango cha juu na asilimia 15, kiwango cha chini.
Komba anasema kama uzalishaji ni mkubwa, basi mgao wa Taifa nao huongezeka na kama ugunduzi ni wa mafuta pia mgawanyo wa Taifa huwa mkubwa zaidi. “Taifa huchukua mgawanyo zaidi katika mafuta, kwa sababu mafuta yanauzika kirahisi zaidi duniani kuliko gesi na pia miundombinu ya kuendeleza mafuta, haihitaji mitaji mikubwa kama ilivyo kwa gesi asilia,” alisema Komba.
Aidha, alisema mpaka kufikia sasa mikataba ya PSA 35 imekwishaingiwa kati ya Serikali, TPDC na wawekezaji na kati ya hiyo, mikataba 22 bado inafanyiwa kazi na kampuni 19 ndizo zinazofanya kazi za utafiti na uendelezaji hapa nchini.
Faida za mkataba Kupitia mfumo huo wa PSA, Komba amesema kampuni au muwekezaji hutumia fedha zake kufanya shughuli zote za awali za utafiti, ikiwa ni pamoja na kukusanya data mtetemo (seismic), ambazo zingine huuzwa na TPDC, kuzifanyia tathmini na kuchimba kisima cha kwanza cha utafiti (exploration well), hatua ambazo ni za gharama kubwa.
Kwa mujibu wa Komba, kama itatokea hakuna ugunduzi katika kisima hicho, basi fedha yote ya mwekezaji iliyotumika katika uwekezaji hupotea na hasara huwa ni ya kwake. Lakini ikitokea ugunduzi umefanyika, Komba amesema muwekezaji atajirudishia sehemu ya gharama alizoingia wakati wa utafiti, baada ya kuanza kuingiza fedha kwa kuuza gesi au mafuta aliyogundua.
Faida nyingine, Komba amesema ni pamoja na rasilimali kubaki kuwa mali ya Taifa, huku kampuni au muwekezaji akibeba hatari ya kuwekeza fedha katika utafiti na kukosa rasilimali. Nyingine, mrabaha hulipwa kwa Serikali mwanzoni kabisa mwa uzalishaji, huku urejeshaji wa gharama za mwekezaji ukiwekewa kikomo cha asilimia 50. “Mfumo huu hutoa fursa kwa Taifa kuanza kupata mapato yatokanayo na uzalishaji wa mafuta au gesi asilia mara tu uzalishaji unapoanza,” alisema Komba.
Urudishaji gharama “Muwekezaji huruhusiwa kujirudishia gharama zake kwa mwaka bila kuzidi asilimia 50 ya gharama zote na faida hugawanywa kati ya muwekezaji na Taifa,” alisema Komba. Kuhusu uwezekano wa Serikali kubambikiwa gharama ambazo hazikuwepo, ili mwekezaji atumie nafasi hiyo kujinufaisha wakati wa kujirudishia gharama, Komba amesema hiyo haiwezekani.
Akifafanua zaidi, Komba amesema Taifa kupitia TPDC, hupitia mpango kazi na bajeti ya kila mwaka ya muwekezaji na kutoa idhini ya mpango kazi na bajeti hiyo kutumika. Baada ya kuidhinisha bajeti ya mwekezaji, Komba amesema pia TPDC, hufanya ukaguzi wa gharama zote ambazo muwekezaji ametumia ambazo atahitaji kuzirejesha uzalishaji utakapoanza.
Naye Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Ndani wa TPDC, Gabriel Mwero, alisema ukaguzi wa gharama anazotumia mwekezaji katika utafiti, hufanyika kwa kila kampuni iliyowekeza katika utafiti hapa nchini. “Aina ya ukaguzi unaofanyika, ni ule wa asilimia 100 na hivyo kuhakikisha kwamba hakuna gharama ambayo haijaangaliwa. Hivyo kampuni hujirudishia zile gharama ambazo zimekaguliwa na TPDC na kuidhinishwa,” alisema.
Je uvunaji umeshaanza Mpaka sasa kwa mujibu wa taarifa za TPDC, kampuni zilizofanya ugunduzi mkubwa katika kina kirefu cha bahari za BG na Statoil, kiasi cha futi za ujazo zaidi ya trilioni 47.8, hazijaanza kuvuna gesi hiyo. Kwa mujibu wa taarifa hizo, uvunaji hauwezi kufanyika bila kujenga mtambo wa kugeuza gesi asilia kuwa kimiminika, ili ifae kusafirishwa ndani au nje ya nchi.
Wiki hii ndio TPDC imetangaza upatikanaji wa hati miliki ya ardhi kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa mtambo huo wa kuchakata na kusindika gesi asilia (LNG), ili iwe kimiminika. Eneo la ardhi hiyo lipo katika kiwanja Na.1-Kitalu “A”, Likong’o katika Manispaa ya Lindi na lilipendekezwa na kuchaguliwa kwa pamoja kati ya TPDC na wawekezaji wa mradi huo.
Sheria kali Kuhusu udhibiti wa mapato, tayari Tanzania ina Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi wa Mwaka 2015, ambayo imeweka adhabu kwa watakaobainika kuchota fedha katika Mfuko wa Mafuta na Gesi utakaoanzishwa na sheria hiyo. Miongoni mwa adhabu hizo ni pamoja na faini isiyopungua kiasi mtu alichochukua au kupoteza, kifungo cha miaka 30 jela na kufilisiwa mali zao.
Kwa mujibu wa Sheria hiyo, Mfuko huo wa Mafuta na Gesi utakuwa na akaunti mbili zitakazotunzwa na kusimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania. Akaunti hizo ni Akaunti ya Kupokea Mapato na Akaunti ya Kutunza Mapato.
Chanzo: HabariLeo