Friday, December 4, 2015

Mkuu wa Makoa Morogoro Amkana Kigogo Sumatra

MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Dk Rajab Rutengwe
MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Dk Rajab Rutengwe ameamuru Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) Mkoa wa Morogoro, Allen Mwanri kurudi kwa mwajiri wake baada ya kile kinachoelezwa kushindwa kudhibiti ukiukwaji wa maadili ya utumishi wa umma na vitendo vya rushwa katika ofisi yake.
Licha ya ofisa huyo kurejeshwa kwa mwajiri wake Sumatra Makao Makuu, ameitaka mamlaka hiyo na nyingine kumchukulia hatua za kisheria na kinidhamu mtumishi mwingine anayedaiwa mzoefu wa kufanya udanganyifu katika utoaji wa leseni kwa kutumia vitabu vya Sumatra na uandishi wake kwenda kinyume cha taratibu na kuagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ichunguze kwa kina suala hilo.
Akizungumza jana mjini hapa, alisema Serikali haiko tayari kumvumilia mtumishi yeyote asiyezingatia uadilifu, uaminifu na weledi ambapo bado watumishi wengine wa taasisi za serikali wanachunguzwa utendaji kazi wao.
Alitoa uamuzi huo baada ya kumalizika kwa mkutano kati yake na wafanyabiashara wa magari ya abiria aina ya Toyota Noah, Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa na Sumatra Mkoa huo kutokana na wafanyabiashara hao kufika ofisini kwake.
Wafanyabiashara hao ambao magari yao yanafanya kazi katika barabara ya Morogoro- Gairo, Morogoro- Turiani na maeneo ya Mjini, walifikisha malalamiko yao kwa mkuu wa mkoa juu ya uonevu, uombaji rushwa unaofanywa na maofisa wa Sumatra Mkoa na Askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani.
Dk Rutengwe alifikia uamuzi wa kumrudisha Ofisa Mfawidhi wa Sumatra Mkoa, Mwanri kwa mwajiri wake makao makuu. Wafanyabiashara hao walidai kuzuiwa kwao kusafirisha abiria hasa katika barabara ya Morogoro- Turiani kulitokana na Sumatra Mkoa kushirikiana na wamiliki wa mabasi makubwa ya abiria wakihusishwa na askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani wa njia hizo.
Mkuu wa Mkoa alisema kumekuwa na udhaifu wa utendaji wa Sumatra Mkoa kutokana na vielelezo vilivyowasilishwa na wafanyabiashara kuonesha kulikuwa na viashiria vya ukiukwaji wa maadili katika ofisi hiyo.
Aidha, ameiagiza Takukuru kuendelea na uchunguzi wa kina kwa kuwa vipo viashiria vya mazingira ya rushwa baada ya kubainika kwa kuonekana leseni zimetolewa kwa kuhusisha vitabu halali vya Sumatra, lakini uandishi ndani ya vitabu hiyo umekwenda kinyume cha taratibu.
Kuhusu askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani wanaolalamikiwa kwenye barabara ya Morogoro- Turiani alimwelekeza Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Leonard Paulo kuchukua hatua.
Chanzo: HabariLeo