Monday, January 25, 2016

BREAKING NEWS: Diwani Afariki Ghafla Shambani

BARAZA la Madiwani wa halmashauri ya Manispaa ya Morogoro limepata pigo kubwa kufuatia Diwani wa Kata ya Kiwanja cha Ndege katika Manispaa hiyo, Godfrey Mkondya (CCM) kufa ghafla akiwa shambani kwake katika Kata ya Mikese iliyopo halmashauri ya wilaya ya Morogoro.
Kifo hicho cha ghafla kimethibitishwa na Kaimu Mganga wa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, Dk Francis Semwene, baada ya kupokewa kwa mwili wa diwani huyo hospitalini hapo akiwa ameshafariki.
Alisema bado mwili wa diwani huyo haujafanyiwa uchunguzi na hilo litafanyika kwa idhini ya wanafamilia iwapo watahitaji mwili wake ufanyiwe uchunguzi.
Kwa mujibu wa ndugu wa karibu na Mkondya akiwemo mama yake mzazi walisema diwani alikufa alfajiri ya Januari 22, mwaka huu wakati akiwa shambani kwake eneo la Mikese wilaya ya Morogoro.
Kwa mujibu wa ndugu wa marehemu, walisema Mkondya aliondoka nyumbani mapema alfajiri kuelekea shambani kwake kwa ajili ya shughuli zake za kila siku na kwamba msiba huo upo nyumbani kwa mama yake mzazi eneo la Mazimbu na familia imefikia uamuzi wa kumzika mjini Morogoro kesho.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Wilaya ya Morogoro mjini, Fikiri Juma alisema, chama na wananchi wa kata hiyo wamepata pigo la kuondokewa na kiongozi wao aliyekuwa mchapakazi hodari na mpenda maendeleo ya wanyonge.
Chanzo: HabariLeo