Monday, January 25, 2016

NEWS: Vigogo Watatu NEMC Wasimamishwa Kazi

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba, amewasimamisha kazi maofisa watatu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
Wanatuhumiwa kukiuka miiko ya kazi katika kusimamia kiwanda cha kusindika minofu ya punda kilichopo mkoani Dodoma.
Maofisa hao ni Ofisa Mazingira Mwandamizi Dk Eladius Makene, Mwanasheria Daraja la II Wakili Heche Suguta Manchare, na Ofisa Mazingira, Boniface Benedict Kyaruzi.
Aidha, Waziri huyo ameagiza Mkurugenzi Mkuu wa baraza hilo, Bonaventura Baya, aandikiwe barua ya onyo kali na la mwisho kwa tuhuma ya udhaifu wa usimamizi wa watumishi wa NEMC, hivyo kusababisha malalamiko mengi kuhusu utendaji wa Baraza hilo.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, January alithibitisha kuchukua hatua hiyo dhidi ya maofisa hao wa NEMC.
Taarifa ambayo gazeti hili linayo kutoka Ofisi ya Wizara hiyo ya Muungano na Mazingira, ilibainisha kuwa uamuzi wa waziri huyo ulitolewa baada ya kikao kilichofanyika Januari 24, mwaka huu kuhusu kuimarisha utendaji ndani ya Baraza hilo.
Kuhusu kiwanda cha kusindika minofu ya punda mkoani Dodoma, taarifa hiyo ilisema imegundulika kuwapo kwa ukiukwaji mkubwa, wa makusudi na wa wazi wa miiko ya kazi kwa watumishi wa NEMC walioshughulika na kiwanda hicho.
Aidha, taarifa hiyo ilisema “Imebainika kwamba usimamizi wa watumishi wa NEMC siyo makini na thabiti na kusababisha malalamiko mengi kuhusu utendaji wa Baraza. Hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Mhandisi Bonaventura Baya apewe barua ya onyo kali na la mwisho kwa udhaifu katika usimamizi wa watumishi wa Baraza”.
Ilieleza kuwa NEMC kama chombo muhimu nchini, kilichopewa jukumu la kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, inatarajiwa kazi zake zifanyike kwa ufanisi wa kiwango cha juu kulingana na majukumu yaliyoko kwenye sheria.
Waziri huyo alisema kutokana na mapungufu yanayojitokeza, ndani ya wiki moja ataunda jopo la wataalamu wasiozidi watano ili kutathmini utendaji wa baraza hilo na changamoto mbalimbali katika usimamizi wa hifadhi ya mazingira na kuishauri serikali ipasavyo.
January alisema ili kuimarisha ufanisi na udhibiti wa utendaji wa NEMC, ndani ya wiki moja pia litatolewa tangazo litakalokuwa na anwani ya barua pepe, nukushi, namba ya simu, namba ya whatsapp ili mtu yeyote mwenye malalamiko au aliyewahi kuombwa rushwa na watumishi wa NEMC, ama kufanyiwa jambo kinyume na maadili ya kazi yao, atoe taarifa mara moja ili uchunguzi ufanyike na hatua zichukuliwe.
Aidha, alisema kutokana na mapungufu yanayojitokeza katika utekelezaji wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira, ndani ya wiki moja NEMC ipitie upya orodha ya wataalamu na taasisi elekezi, zilizosajiliwa na kufuta wataalamu na taasisi zote ambazo zimekuwa zikikiuka maadili ya kazi zao.
Alitaja baadhi ya ukiukwaji unaofanywa na baadhi ya taasisi hizo kuwa ni pamoja na kuwasilisha taarifa zilizo chini ya viwango, kuchelewesha kazi za wateja wao na kutowasiliana na wateja wao kuhusu hatua za utekelezaji wa maombi yao.
Pia, January alilitaka baraza hilo kuitisha mkutano wa dharura wa Bodi ya NEMC ndani ya wiki tatu, kujadili na kufanya maamuzi juu ya changamoto za utendaji katika baraza hilo.
Chanzo: HabariLeo