Saturday, January 2, 2016

Kova Asimulia Jinsi Magufuli, Lowasa Walivyomtesa

 ALIYEKUWA Kamanda wa Polisi katika Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova amestaafu rasmi na kuagwa jana huku akikiri kuwa hatasahau joto la uchaguzi mkuu 2015 lililosababishwa zaidi na mchuano wa wafuasi wa wagombea urais John Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Edward Lowassa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
 
Akizungumza wakati wa kuagwa kwake na kisha kukabidhi majukumu kwa kamanda mpya wa kanda hiyo, Naibu Kamishna wa Polisi, Simon Sirro, Kova alisema uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 25, 2015 ni miongoni mwa vipindi vitatu asivyotarajia kuvisahau katika maisha yake yote ya kulitumikia jeshi la polisi.
 
Alivitaja vipindi vingine asivyovisahau wakati akilitumikia jeshi la polisi katika Kanda Maalum ya Dar es Salaam kuwa ni tukio la kuvamiwa kwa kituo cha polisi Stakishari lililoacha vifo kwa baadhi ya askari wake na pia ajali ya helikopta. 
 
Akieleza zaidi kuhusiana na uchaguzi mkuu, Kova alisema uchaguzi huo ulimpa changamoto kubwa kutokana na wagombea hao kuungwa mkono na watu wengi kiasi cha kuhofia kutokea machafuko, hasa kutokana na kuwapo kwa mwamko mkubwa wa kisiasa miongoni mwa wafuasi wa wagombea.
Hata hivyo, Kova alisema anashukuru kuwa serikali iliwaunga mkono vya kutosha katika kulinda usalama na hivyo kufanikisha uchaguzi huo kwa ufanisi.
“Napenda kuishukuru serikali kwa ushirikiano mkubwa waliotupatia jeshi la polisi wakati  wa uchaguzi kwa kutuongezea vifaa vya kazi kama magari ya kufanyia doria, silaha pamoja, kwani vilituwezesha  kufanikiwa kulinda amani na utulivu wa hali ya juu,” alisema Kova.
 
AMTAMBULISHA KAMANDA SIRRO 
Katika hatua nyingine, Kamanda Kova alimtambulisha rasmi jana Naibu Kamishna wa Polisi Sirro, kuwa mrithi wa wadhifa wake.
Akiongea na waandishi wa habari juu ya hatua hiyo, Kova alisema kwake yeye, kukabidhi madaraka kwa Kamanda Sirro ni kitendo cha kihistoria kwani ilikuwa ni ishara ya kuhitimisha salama utumishi wake ndani ya jeshi hilo. 
“Ni siku  ya kihistoria katika maisha yangu kutokana na tendo hili. Lakini naahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa kila namna kwa Kamishna  Sirro,” alisema

Chanzo: Nipashe