Saturday, January 2, 2016

Naibu Waziri Tanzania Awanyoosha Afya

Watumishi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wameanza kutii agizo la Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Hamis Kigwangalla, la kufika ofisini kabla ya saa 1:30 ikiwa ni utaratibu uliopangwa na serikali kwa watumishi wote wa umma nchini.
 
Uchunguzi uliofanywa na Nipashe ili kubaini iwapo agizo la Naibu Waziri alilotoa baada ya kuwafungia nje wachelewaji lango kuu wiki mbili zilizopita limetekelezwa, ulibaini mambo chanya.
Uchunguzi huo wa hivi karibuni wa Nipashe umebaini watumishi wa wizara hiyo wamekuwa wakifika kazini kwa muda unaotakiwa ili kukwepa kufungiwa nje kama ilivyowahi kutokea.
 
Mmoja wa wahudumu wa Wizara hiyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe na Nipashe kwa sababu si msemaji, alisema hivi sasa watumishi wengi wanafika kabla ya muda huo wa saa 1:30, kwani inapofika saa mbili hakuna pilika pilika za watumishi hao kuingia ndani ya Wizara hiyo.
 
Alisema ingawa watumishi hao wamekuwa wakiwahi kwa muda uliopangwa, wageni ambao hufika kwa ajili ya kuhudumiwa au kufuatilia masuala mbalimbali wizarani hulazimika kusubiri hadi saa 3:00 asubuhi ndipo waruhusiwe kuingia.
 
“Kama ni mgeni unakaa hapo getini ukisubiri hadi ifike saa 3:00 asubuhi ndipo uhudumiwe, siyo, watumishi wanakuwa ndani na kwa kweli agizo la waziri limefanya kazi,” kilisema chanzo hicho.
 
Aidha, baadhi ya wakuu wa idara, vitengo ambao hawakutaka majina yao yaandikwe gazetini, walisema watumishi wengi wanawahi kufika ofisini tofauti na hapo awali ambapo wengine walikuwa wakifika saa 3:00 au saa 4:00.
 
“Siku hizi kama mtumishi akichelewa siku hiyo ujue ameshawasiliana na bosi wake, yaani Mkuu wa Idara kwa kutoa sababu za kuchelewa kwake,” alisema mmoja wa wakuu wa vitengo wizarani hapo ambaye hakutaja jina lake litajwe pia.
 
Desemba 18 mwaka jana, Naibu Waziri Dk. Kingwangalla alisimama getini na kuwafungia nje watumishi wote wa wizara hiyo waliofika ofisini baada ya saa 1:30 asubuhi muda ambao ndiyo mwisho wa watumishi kuingia ofisini.
 
Dk. Kigwangalla alifika wizarani hapo saa 1:05 asubuhi na ilipofika saa 1:30 alisimama getini na kisha kuwaamrisha walinzi kulifunga geti hilo na wasiruhusu mtu yeyote kuingia ndani, ili kubaini watumishi wanaochelewa kufika ofisini.
 
“Fungeni geti na kila atakayefika msimruhusu kuingia ndani maana ninataka kuona wote ambao wamechelewa,” alisikika Dk. Kingwangalla akiwaambia walinzi.

Chanzo: Nipashe