Friday, February 12, 2016

Kenya yashindwa kutimiza masharti ya riadha

 Kenya imeshindwa kuafikia mda wa masharti yaliowekwa kwa taifa hilo kudhihirishia duniani kwamba inakabiliana na udanganyifu katika riadha.
Kenya haikuweza kutoa thibitisho kwa shirika la kukabiliana na utumiaji wa dawa za kusisimua misuli duniani Wada na kwamba huenda ikaorodheshwa miongoni mwa mataifa yaliopo katika hatari ya kukiuka sheria ya shirika hilo.
Taifa hilo la Afrika mashariki ,ambalo wanariadha wake wametawala katika mbio ndefu duniani ,litapewa miezi miwili kuanzisha sheria na ufadhili la sivyo liorodheshwe miongoni mwa mataifa ambayo hayajatimiza matakwa ya Wada
Hii itamaanisha kwamba huenda likapigwa marufuku kushiriki katika mashindano ya Olimpiki,ambayo yatafanyika baadaye mwaka huu nchini Brazil,pamoja na michezo mingine mkubwa.
Taarifa ya Wada imesema kuwa huku ikiwa hatua zimepigwa na shirika la Kenya linalokabiliana na utumizi wa dawa za kusisimua misuli ,kuna kazi zaidi inayohitajika.