Monday, March 14, 2016

Mkandarasi wa umeme aumbuliwa

WANANCHI wa vijiji vya Kahe-Useri na Ngaseni kata ya Ubetu Kahe wilayani Rombo, mkoani Kilimanjaro wamekataa taarifa za mradi wa umeme vijijini (REA), unaotekelezwa na kampuni ya Spencon ya Dar es Salaam kwa madai unafanyika kwa ubaguzi na misingi ya rushwa.
Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa mkoa huo, Amos Makalla ameagiza kufanyika kwa kikao cha utambulisho kitakachohusisha wafanyakazi wa Shirika la Umeme nchini(Tanesco) wilaya ya Rombo ili kuwatambua watumishi waliokuwa wakichukua Sh 30,00 kama rushwa kwa wananchi, ikiwa ni sharti la kufungiwa umeme.
Katika mikutano ya hadhara iliyofanyika katika vijiji hivyo, Mkuu wa mkoa alikuwa na lengo la kukagua utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi wa umeme vijijini pamoja na kukabili changamoto zinazojitokeza.
“Wote mmesikia mkandarasi na Tanesco katika wilaya hii mnalalamikiwa kuchukua Sh 30,000 kwa zaidi ya watu 44 wanaohitaji umeme, nataka Jumatatu (leo) mfanye utambulisho kwa wafanyakazi ili wananchi wawabainishe wanaochukua rushwa,”alisema.
Alimtaka mkuu wa wilaya hiyo, Lembris Kipuyo kuongoza utambulisho huo ili kuhakikisha wananchi hawanyanyaswi kwa misingi ya rushwa, jambo linalochangia kuichukia serikali yao. Makalla alihoji kama gharama za fomu ya maombi ya kuunganishiwa umeme ni Sh 5,900 kwa nini wafanyakazi hao wawatoze wananchi kiasi kikubwa cha fedha ambacho kinaweka daraja baina ya masikini na tajiri.
Mkuu wa mkoa alikuwa akizungumzia hoja za baadhi ya wananchi, Richard Uiso na Merina Shirima waliodai mradi huo wa umeme umeelekezwa kwa watu wenye uwezo kiuchumi, licha ya kwamba walistahili kupata wao ambao wapo katika njia kuu zilizoainishwa katika mradi huo.
“Mkuu wa mkoa huyu mkandarasi na hawa wafanyakazi wa Tanesco wanasema uongo lakini wamepeleka umeme kwa matajiri licha ya kwamba walitutoza Sh 30,000,” alisema. Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Rombo, Joseph Selasini alisema alipewa malalamiko kwamba mkandarasi kampuni ya Spencon amebadili njia ya kupitisha umeme na kuwafungia wateja 167 ambao asilimia kubwa wamepewa kwa misingi ya rushwa.
“Hao wote wanaotajwa kufungiwa umeme ni wale wenye uwezo na hawakuwa katika mradi...huyu mkandarasi amechepusha mradi kufuata matajiri, ili kuepusha yote haya atuoneshe makisio ya tathmini ya mradi (BOQ) tutazame njia zilizotajwa katika mradi,” alisema.
Akijibu tuhuma za rushwa, Kaimu Meneja wa Tanesco mkoani hapa, Fataely Maro alisema wanatekeleza mradi kwa mujibu wa sheria na siyo vinginevyo. Naye msimamizi wa mradi huo kutoka kampuni ya Spencon, Bumarwa Mushumbuzi alisema katika kijiji cha Kahe amejenga umeme wa msongo mkuu kwa umbali wa Km 3.1 na amefunga Transfoma yenye uwezo wa KVA 100.
Kazi nyingine ni kufunga mtandao mdogo wa umeme kwenda kwa wateja Km 3.8, umeme mdogo kwa ajili ya mashine Km moja na kufunga mita kwa wateja 167, taarifa ambayo ilipingwa na wananchi hao.
Chanzo: HabariLeo