Tuesday, March 15, 2016

Mtumishi wa ndani ajiua kwa khanga


By Hamida Shariff, Mwananchi
Mtumishi wa kazi za ndani aliyejulikana kwa jina la Rehema, amekutwa amekufa kwa kujinyonga kwa khanga chumbani kwake kwenye nyumba ya mwajiri wake katika Mtaa wa Ngazengwa, Kata ya Kiwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro.
Mwajiri wa mtumishi huyo, Said Kulunge alisema kuwa kifo hicho kiligundulika jana asubuhi.
Kulunge alisema mtumishi huyo anayekadiriwa kuwa na miaka kati ya 17 hadi 19 alianza kufanya kazi nyumbani kwake wiki mbili zilizotopita baada ya kuletwa kutoka Mang’ula wilayani Kilombero.
Alisema baada ya mtumishi huyo kuchelewa kuamka jana asubuhi, alikwenda kumuamsha chumbani kwake na kukuta mlango umefungwa kwa ndani.
Kulunge alisema baada ya kugonga bila mafanikio, alichungulia kwenye matundu yaliyopo kwenye mlango huo na kushuhudia mwili wa mtumishi huyo ukining’inia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo, alisema bado wanaendelea kufanya uchunguzi wa kifo hicho ili kubaini chanzo chake.
“Katika uchunguzi wa awali tumegundua kuwa binti huyo alifunga mlango kwa ndani kabla hajajinyonga hakuacha ujumbe wowote, hivyo kwa mazingira haya tunaendelea kufanya uchunguzi,” alisisitia Paulo.
Kamanda huyo alisema polisi wamemuhoji mwajiri wa mtumishi huyo kuhusiana na kifo hicho.
Alisema mwili wa marehemu huyo umehifadhiwa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro kwa uchunguzi zaidi wa madaktari.

HABARI NA MATUKIO ZAIDI YA KUSISIMUA CLICK HAPA>>