Washtakiwa wengine ni mfanyabiashara Kanji Mwinyijuma na Katibu wa Rahco, Emmanuel Massawe.
Walisomewa mashitaka yao jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Upande wa Jamhuri uliongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Timon
Vitalis, akisaidiana na Waendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru), Janeth Machurya, Maghela Ndimbo na
Stanley Luoga.
Vitalis alidai kuwa kati ya Septemba Mosi, 2014 na 30, 2015, jijini
Dar es Salaam, washtakiwa wote kwa pamoja walikula njama ya kutenda
makosa kinyume cha Sheria ya Takukuru ya mwaka 2007.
Katika shitaka la pili, ilidaiwa kuwa Februari 27, mwaka 2015,
katika ofisi za Rahco zilizopo Ilala, mshtakiwa Tito akiwa kama
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, alitumia madaraka yake vibaya kwa
kuiajiri kampuni ya Rothschild (Afrika ya Kusini) Proptietary Limited.
Ilidaiwa kuwa mshtakiwa wa kwanza aliiajiri kampuni hiyo kama
mshauri wa mradi wa uimarishaji Reli ya Kati bila idhini ya Bodi ya
Zabuni ya Rahco kinyume cha Sheria za Manunuzi ya Umma.
Wakili huyo alidai katika shitaka la tatu, mshtakiwa wa kwanza na
wa tatu, walitumia madaraka yao vibaya kwa kusaini barua ya kumpitisha
na kuhalalisha kampuni ya Afrika Kusini kutoa huduma za ushauri wa
kifedha kuhusiana na huo mradi.
Shitaka la nne, kati ya Machi 12 na Mei 20, mwaka 2015, Wilaya ya
Ilala, washtakiwa walitumia madaraka yao vibaya kwa kushindwa kutimiza
majukumu yao kwa kuwasilisha mkataba wa huduma ya ushauri kati ya
kampuni ya Afrika ya Kusini na Rahco kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali
(AG) kinyume cha sheria ya manunuzi.
Upande huo wa Jamhuri ulidai katika shitaka la tano, Mei 20, mwaka
2015 mshtakiwa wa kwanza na wa tatu, katika ofisi za Rahco, walitumia
madaraka yao vibaya kwa kusaini mkataba kati ya Kampuni ya Afrika ya
Kusini na Rahco bila kibali cha Bodi ya Zabuni kinyume cha sheria ya
manunuzi ya umma.
Ilidaiwa katika shitaka la sita, kati ya Mei 20 na Juni 20, mwaka
2015 katika ofisi za Rahco mshtakiwa wa kwanza na wa tatu, walitumia
vibaya madaraka yao kwa kushindwa kuwasilisha nakala ya mkataba
uliofanywa Mei 20, mwaka 2015 kwa AG na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
kinyume na sheria za manunuzi ya umma.
Ilidaiwa katika shitaka la saba, kati ya Machi na Septemba, 2015
katika ofisi ya Rahco washtakiwa wote watatu waliisababishia Kampuni ya
Rahco hasara ya Dola 527,540 za Marekani kama malipo ya awali na tozo la
benki la kuhamisha.
Wakili huyo aliendelea kuwasomea washtakiwa kwamba, Agosti 18,
mwaka 2015 katika ofisi za Rahco, mshtakiwa wa kwanza alitumia madaraka
yake vibaya kwa kutoa zabuni ya kujenga kilomita mbili za reli ya kati
kwa gharama ya Dola 2,312,229.39 za Marekani bila kibali cha Bodi ya
Zabuni ya Rahco kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya Umma.
Hata hivyo, kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi
za uhujumu uchumi, washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote hadi
upelelezi utakapokamilika itahamishiwa Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya
Dar es Salaam kwa ajili ya kusikilizwa.
Hata hivyo, Wakili wa Utetezi, Melikiori Sanga, alidai kuwa kesi
inayowakabili washtakiwa ina dhamana na kwamba mahakama hiyo ina mamlaka
ya kutoa dhamana.
Lakini upande wa Jamhuri ulidai kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya
kutoa dhamana ya makosa ya uhujumu uchumi na kwamba itupilie mbali
maombi ya utetezi.
Hakimu Simba alisema baada ya kusikiliza hoja za kisheria za pande
zote mbili, mahakama itatoa uamuzi kama washtakiwa watasikilizwa maombi
ya dhamana ama la, Machi 18, mwaka huu.
Washtakiwa walipelekwa mahabusu hadi Machi 18, mwaka huu.
Chanzo: Nipashe