Thursday, March 31, 2016

UKATILI: Mtoto afungiwa ndani na kunyimwa huduma muhimu za kibinadamu.


Mtoto Bahati Ally Kaminyoge mwenye umri wa miaka 12 amefanyiwa ukatili wa kutisha na wazazi wake baada ya kufungiwa ndani ya nyumba kwa zaidi ya miaka 10 bila kutoka nje,huku wakimnyima baadhi ya huduma muhimu za kibinadamu.

Taarifa za ukatili dhidi ya mtoto huyo zimetolewa na raia wema ambao wamezifikisha kwa Mwenyekiti wa kituo cha haki za kibinadamu mkoani Mbeya, Said Mohamed Madudu ambaye ameshirikiana na Ofisi ya Maendeleo ya Jamii wilayani Mbozi pamoja na Jeshi la Polisi kufika katika kijiji cha Mbimba kitongoji cha Isinizya wilayani Mbozi na kumkuta mtoto huyo akiwa hoi bin taaban.
 
Wakati mtoto huyo akitolewa ndani ya nyumba alimofungiwa, wazazi wake wote hawakuwepo nyumbani, na ikaelezwa kuwa mama yake mzazi alikuwa shambani, ambapo alifuatwa na alipoletwa alidai kuwa mwanaye alizaliwa akiwa na uzito mdogo na baadaye alielezwa hospitalini kuwa mtoto huyo ni mlemavu wa akili.

Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Ahamed Namohe amesema kuwa matukio ya ukatili wa watoto wilayani mwake ni makubwa na kwamba kufichuliwa kwa matukio hayo kunatokana na elimu ya kupinga ukatili huo ambayo imeanza kutolewa wilayani Mbozi kwa kushirikiana na kituo cha haki za binadamu.
 
Mama mzazi wa mtoto huyo ameshikiliwa katika kituo cha Polisi cha Vwawa wilayani Mbozi akisubiri kuchukuliwa hatua za kisheria kutokana na ukatili huo.

Chanzo: ITV