Friday, April 15, 2016

Magufuli atengua uteuzi wa Nderumaki

Aliyekuwa Mhariri Mtendaji wa TSN, Gabriel Nderumaki
RAIS John Magufuli ametengua uteuzi wa Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Gabriel Nderumaki ; na amemteua Tuma Abdallah kukaimu nafasi hiyo. Februari 22, mwaka huu, Bodi ya Wakurugenzi ya TSN ilimsimamisha kazi Mhariri Mtendaji huyo, muda mfupi baada ya ziara ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye aliyefika kwenye kampuni kuangalia namna ya kuboresha utendaji wa kazi.
Taarifa iliyotolewa jijini Dar es Salaam jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijaziilieleza kuwa Rais Magufuli ametengua uteuzi huo kuanzia Machi 18, mwaka huu. Balozi Kijazi alisema kutokana na kutenguliwa kwa uteuzi huo, Rais Magufuli amemteua Tuma Abdallah kukaimu nafasi hiyo hadi hapo uteuzi mwingine utakapofanyika. Tuma ni Naibu Mhariri Mtendaji wa TSN.
Februari 22, mwaka huu, kabla ya uamuzi wa Bodi kufanyika, Nape alizungumza na Menejimenti katika kikao cha ndani na kisha akaitaka Bodi ya Wakurugenzi ya TSN iliyo chini ya Mwenyekiti Profesa Moses Warioba kukaa kupitia hoja zilizoibuka kwenye kikao hicho.
Nape alisema kutokana na ripoti, amebaini kuwapo matatizo makubwa, ikiwemo kukosekana mawasiliano kati ya Bodi na Menejimenti. Pia alisema alibaini utendaji mbovu wa menejimenti, uliochangia kushusha ari ya kazi ya wafanyakazi.
Baada ya kikao cha Bodi cha takribani saa mbili, Mwenyekiti wa Bodi, Profesa Warioba alisema wameamua kumsimamisha kazi Nderumaki kupisha uchunguzi ambao utafanywa na Serikali.
Aidha, wakati ule Bodi ikimsimamisha kazi Mhariri Mtendaji, pia ilitengua uteuzi uliofanywa na Mhariri Mtendaji huyo kwa Madiya Magesa, aliyekuwa Kaimu Meneja wa Kiwanda wakimtaka arejee katika nafasi yake ya Uhasibu kutokana na kukosa sifa.
Magesa alipewa wadhifa huo kutokana na kusimamishwa kazi kwa Meneja wa Kiwanda, John Mcharo. Hata hivyo, Warioba alisema taratibu za kisheria, zitafuata katika kumpata mtu atakayeshika wadhifa huo.
Pia Bodi ilitengua uteuzi wa Felix Mushi, aliyeshikilia nafasi ya Kaimu Meneja Mauzo na Masoko kwa kusema mbali na kutokuwa na sifa, pia uadilifu wake unatiliwa shaka. Awali, Mwenyekiti wa Bodi, Profesa Warioba alisema Waziri Nape alitoa maelekezo ya mambo mengi, yaliyotakiwa kufanyiwa kazi ikiwamo kutokuwapo kwa maelewano kati ya Menejimenti, wafanyakazi na Chama cha Wafanyakazi (RAAWU).
Mengine ni baadhi ya wafanyakazi kupewa majukumu ambayo hawana sifa, kumsimamisha kazi meneja wa kiwanda bila kufuata taratibu na kuangalia sababu za wafanyakazi zaidi ya 21 kuacha kazi katika kipindi cha muda mfupi. TSN huchapisha magazeti ya Daily News, Sunday News, HabariLeo na SpotiLeo.