Monday, April 18, 2016

Simba Fungu la Kukosa

INAWEZA kuwa fungu la kukosa kwa Simba baada ya kupoteza kwa bao 1-0 mechi dhidi ya Toto Africans na hivyo kutia ugumu mbio zake za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Simba ilihitaji ushindi katika mechi hiyo ya jana ili kulingana pointi na Yanga kwenye mbio za ubingwa.
Yanga inaongoza msimamo ikiwa na pointi 59 na Simba ikiwa nafasi ya pili kwa pointi 57.
Ni fungu la kukosa kwa Simba baada ya kutolewa kwenye michuano ya kombe la Shirikisho na hivyo nafasi pekee ya timu hiyo kushiriki kwenye michuano ya kimataifa kubaki kwenye Ligi Kuu.
Toto Africans ilipata bao lake katika dakika ya 20 likifungwa na Waziri Junior aliyeunganisha pasi ya Edward Christopher na kupiga shuti kali akiwa nje ya 18 na mpira kujaa wavuni.
Simba sasa ina kazi ya ziada kuifukuzia Yanga katika mbio hizo za ubingwa, jambo ambalo linaonekana gumu kutokana na ubora wa Yanga.
Pamoja na bao hilo la kipindi cha kwanza, Simba bado walionekana kutawala mchezo huo hasa kwenye kipindi cha kwanza.
Mechi hiyo ilizidi kuwa mbaya kwa Simba pale mwamuzi Ahmad Simba alipomtoa kwenye benchi kocha Jackson Mayanja baada ya kumfokea dakika ya 30.
Dakika saba baadae, Hassan Kessy alishindwa kuisawazishia Simba bao akiwa amebaki pekee na kipa wa Toto lakini shuti lake lilipanguliwa.
Kipindi cha pili kilianza vibaya kwa Simba baada ya mwamuzi Simba kumtoa Kessy kwa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu Christopher katika dakika ya 47.
Baada ya mechi hiyo, mashabiki wa Simba walimfuata Mwenyekiti wa kamati ya usajili, Zacharia Hanspoppe na kumlaumu kwa kusajili timu mbaya isiyo na wachezaji wenye uwezo.
Mashabiki hao walimrushia Hanspoppe michanga jambo lililomfanya kushindwa kuvumilia na kuingia ndani ya gari yake ambapo alitoa bastola kiunoni na kuiweka kwenye kiti kisha kuendesha gari kwa kasi.