Wednesday, June 29, 2016

Ajali ya basi yaua watano

WATU watano wamekufa baada ya basi aina ya Super Sami, mali ya Kampuni ya Super Sami lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Mwanza, kugonga jiwe na kupinduka katika barabara ya Mwanza-Shinyanga eneo la Mabuki wilayani Misungwi mkoani Mwanza.
Basi hilo lenye namba za usajili T499 BCB, likiendeshwa na dereva William Elias maarufu kama Massa (44) ambaye ni mkazi wa Mabibo jijini Dar es Salaam, lilipata ajali hiyo saa saba usiku wa kuamkia jana.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema baada ya kugonga jiwe dereva alishindwa kulimudu na kupinduka na kusababisha vifo vya watu watano akiwemo dereva, msaidizi wake na majeruhi 13.
Alisema chanzo cha ajali hiyo ni dereva aliyekuwa kwenye mwendokasi hali iliyosababisha basi hilo kugonga jiwe lililokuwa barabarani na kushindwa kumudu basi hilo lililoserereka na kupinduka.
Aliwataja waliokufa kwenye ajali hiyo kuwa ni Massa ambaye ni mkazi wa Dar es Salaam, Vaileth Odede (21) mkazi wa Mwanza, mwanamume mmoja na wanawake wawili wenye umri kati ya miaka 25-30 ambao hawajatambulika.
“Majeruhi watano kati ya 13 wamepelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando kupatiwa matibabu, na wengine wanane wanatibiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Misungwi,” alisema Kamanda Msangi.
Aliwataja majeruhi wanaoendelea na matibabu katika Hospitali ya Misungwi kuwa ni Sophia Miraji (25), Kibilo Mwacha anayekadiriwa kuwa na miaka kati ya 35 hadi 40, Boniphace Charles (38-40) na Frank Munyuni (30).
Majeruhi wengine ni Stanley Zacharia (25), Sia Dauson (28), Hellen Luheke( 30-35), Michael Leonard (30-35), Kudra Ibrahim ambaye ni mtoto wa miaka miwili na miezi 10, Zamda Issa (24), Marietha Christopher (26), Elizabeth Simon (40) na Dickson Msamba (22).