Wednesday, June 29, 2016

Mfanyabiashara achinjwa shingo kwa kudai fedha zake

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Simon Haule

MFANYABIASHARA wa ng’ombe, William Clement (54) mkazi wa Kijiji cha Ihanja Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, ameuawa kwa kuchinjwa shingo kutokana na kumdai mtu mmoja wa kijiji cha jirani Sh 400,000.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Simon Haule alisema mauaji hayo yametokea Juni 22, mwaka huu ambako Clement aliaga nyumbani kwake saa 1.30 usiku kuwa anaenda kwa Hassan Abdallah (38) wa Kijiji cha Mpetu wilayani humo kumdai deni lake la Sh 400,000.
Haule alisema ilipofika saa 5:35 usiku, mfanyabiashara huyo alituma ujumbe mfupi wa simu kwa mtoto wake aitwaye Faraja kumjulisha kuwa alikuwa anarejea nyumbani lakini kulikuwa na watu waliokuwa wanataka kumdhuru hivyo akamtaka aende haraka kumsaidia.
Alisema kwa bahati mbaya Faraja hakuuona ujumbe huo hadi kesho yake ambako alitoa taarifa kwa majirani na msako mkali wa kumtafuta ulianza mara moja na mwili wa marehemu kugundulika ukiwa umefichwa chini ya daraja katika Barabara ya Iseke – Ihanja katika Kijiji cha Iseke.
Kaimu Kamanda alisema tayari Polisi imeshamkamata mtuhumiwa, Hassan Abdalllah na kwamba baada ya mahojiano atafikishwa mbele ya mahakama ili kujibu shitaka linalomkabili.