Saturday, June 4, 2016

Mwanafunzi darasa la sita adaiwa kujinyonga Songea


Songea. Mwanafunzi mwenye umri wa miaka kumi na moja anayesoma darasa la sita, Gloria Mrope amekutwa amekufa huku mwili wake ukining’inia kwenye mti nje ya nyumba ya wazazi wake.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Zuberi Mwombeji alisema mwanafunzi huyo alikuwa akisoma Shule ya Msingi Mashujaa iliyopo Mahenge, Songea inadaiwa kuwa alikufa kwa kujinyonga juzi saa 12:00 jioni.
Alisema baada ya mwili wa Gloria kugundulika, uongozi wa Serikali ya mtaa na Kituo Kikuu cha Polisi cha mjini Songea ulipata taarifa za tukio hilo.
Alisema baadaye polisi walifika eneo la tukio na kueleza watafanya uchunguzi wa tukio hilo, licha ya taarifa za awali kudai hakukuwa na tatizo lolote kwenye familia kabla ya kifo hicho.
Katika tukio jingine, polisi mkoani Ruvuma wanamshikilia Adriano Mpepo (27), mkazi wa kijiji cha Ndongosi wilayani Songea kwa tuhuma za mauaji ya Autani Nyika katika ugomviuliotokea wakati wakinywa pombe.
Kamanda Mwombeji alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 5:00 asubuhi katika kijiji hicho kilichopo karibu na mpaka wa Tanzania na Msumbiji.
Alisema Nyika alifariki dunia akiwa katika Zahanati ya Kijiji cha Ndongosi ambako alikuwa amekwenda kutibiwa kutokana na kipigo.