Thursday, August 4, 2016

Imani za kishirikina.........Anaswa mlangoni Kwa Sangoma

GEITA: MTU mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Mlinda Kioga (38) mkazi wa Kata ya Majengo, Kahama mkoani Shinyanga amekutwa amenasa mlangoni mwa nyumba ya mganga wa kienyeji, tukio lililohusishwa na imani za kishirikina.

Inadaiwa mtu huyo alikwenda katika nyumba hiyo Julai 27, mwaka huu kwa shida ambazo hazikufahamika na akapokewa na mkewe kabla ya mgeni huyo kuomba hifadhi ya kulala, ambapo alioneshwa chumba cha kulala.

Mashuhuda wanasema kesho yake asubuhi, wakati wakipita eneo hilo, mtu huyo alipiga kelele kuomba msaada wa kumnasua, lakini walipojaribu kumsaidia walishindwa. Inadaiwa mgeni huyo alitoka usiku kwa lengo lisilofahamika, lakini akajikuta ameganda mlangoni hadi kesho yake.

“Nilipofika mlangoni niliona giza nene, sikuweza kurudi chumbani wala kutoka nje, ilibidi nijishikize kwenye mlango hadi kulipokucha, nimekesha nimesimama kama unavyoona, sikuweza hata kuchuchumaa wala kuegesha ubavu wangu, naombeni tu msaada wenu,” alisema Kioga akiwa mlangoni hapo.

Baada ya kushindwa kumnasua, mashuhuda hao waliomba msaada wa mjumbe wa nyumba kumi, Helena Joel ambaye naye alishangazwa na tukio huku akimtaja mganga huyo kuwa ni mzee Maziku Makwaya. Yeye ndiye aliyewaita polisi waliofanikiwa kumtoa mtu huyo mlangoni.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ASP Murilo Jumanne amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kama chombo cha usalama, hakiamini imani za kishirikina.