Thursday, August 4, 2016

Undani wa Afisa wa serikali kuuwawa kikatili!

 Marehemu enzi za uhai wake
Manyara:  Afisa Uchunguzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, Evangeline Samson (pichani) aliyeuawa kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana akiwa nyumbani kwake, undani wa kifo hicho umesimuliwa, Chanzo chetu kinakupa zaidi.

Marehemu alifikwa na mauti hayo, usiku wa Julai 24, mwaka huu ndani ya nyumba yake iliyopo katika Mtaa wa Bomani, Manispaa ya Kiteto.

Chanzo cha mauaji hayo kinatajwa kuwa ni wivu wa kimapenzi lakini bado suala hilo lipo chini ya uchunguzi wa polisi kuwabaini wauaji hao na tayari wameshakamatwa watuhumiwa watano.
Ibada ya Mazishi
 
Miongoni mwa waliokamatwa, ni pamoja na mchumba wa marehemu aliyejulikana kwa jina la Talenty, fundi wa gari lake (hakujulikana jina), mtu mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Mkenya na mlinzi huku uchunguzi ukiwa bado unaendelea.

Kwa mujibu wa chanzo cha karibu, kabla ya kukutwa na mauaji, marehemu alikuwa amekaa sebuleni ambapo zilikutwa glasi mbili za pombe kali na sahani mbili za wali na nyama ulioliwa na kubakizwa.
“Mezani kulikutwa glasi mbili za kinywaji kikali. Sasa hatujui kama marehemu alikuwa anakunywa kinywaji hicho na mtu mwingine au la,” alisema mmoja wa mashuhuda ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.
Naye jirani mmoja ambaye pia aliomba hifadhi ya jina lake gazetini, alisema siku moja kabla ya tukio hilo, marehemu alikuwa akilalamika kutojisikia vizuri.

“Nilipomuuliza kama anaumwa, alisema haumwi bali anajisikia kama amefanya jambo baya ambalo litamuingiza hatiani. Nilimuuliza kama aligombana na mtu wake wa karibu, akasema hakuna.
“Kusema ukweli mpaka inafika usiku, marehemu hakuwa sawa. Nadhani kiroho alikiona kifo chake ila alishindwa kukitafsiri,” alisema jirani huyo.
Wafanyakazi waliokuwa wakifanya kazi na marehemu, walisema wanaamini kuna kisasi kilichosababisha kifo cha mwenzao lakini hawajui kama ni kuhusu mapenzi au kazi.

“Kuna kisasi tu lakini vigumu kujua kama ni mapenzi au kazi. Polisi wanachunguza, watasema walichokipata. Ila kusema ukweli mwenzetu amekufa kifo kibaya sana,” alisema mfanyakazi mmoja.
Wakati wa kuaga mwili wa mwanamke huyo, kila mtu alikuwa akisema lake lakini walichokilenga wengi ni kuwa, mauaji hayo yana kisasi ndani yake.
Mtuhumiwa
 
Chanzo chetu kilipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, ACP Francis Massawe, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa, wanawashikilia watuhumiwa watano.
Marehemu ameacha mtoto mmoja, Ethani (7). Alitarajiwa kuzikwa Jumatano iliyopita nyumbani kwao, Ilongero, Singida.
Hadi anakutwa na mauti, marehemu alikuwa akiishi peke yake baada ya kuachana na mume wake wa ndoa miaka michache iliyopita.
 Chanzo: Uwazi